January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Maendeleo yapata faida nono

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

BENKI ya Maendeleo imefanikiwa kupata faida ya sh. bilioni 1.3 kutoka sh. milioni 587 mwaka 2021, ambayo ni sawa na ongezeko la zaidi ya mara mbili ya faida hiyo.

Faida hiyo imetokana na ukuaji wa jumla wa mapato kwa asilimia 22 mwaka hadi mwaka kutoka sh. za kitanzania bilioni 12.8 hadi sh. Bilioni 15.6 mwaka 2022.

Hayo aliyasema jana Jijini Dar es Saalaam, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dkt Ibrahim Mwangalaba wakati akitoa tathmini ya ukuaji wa benki hiyo kwa mwaka 2022.

Alisema kuwa mapato halisi yaliongezeka Kwa asilimia 31 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 7.6 mwaka 2021 hadi shilingi za kitanzania Bilioni 9.9 mwaka 2022,pamoja na biashara ya mikopo kutokana na kuimarika Kwa hali ya uchumi na kuboresha ubora wa vitabu vya mkopo kutoka mikopo chechefu asilimia 13 mwaka 2021 hadi asilimia 5.2 mwaka wa 2022.

“Amana za wateja ziliongezeka kwa asilimia 11 kutoka sh. Bilioni 70 mwaka 2021 hadi shilingi za kitanzania 77 mwaka 2022 wakati mikopo na malipo ya awali kwa wateja yaliongezeka Kwa asilimia 5 kutoka shilingi za kitanzania Bilioni 57 Hadi shilingi za kitanzania Bilioni 60 mwaka 2022” amesema Dkt Mwangalaba.

Aidha alisema mwaka 2022 benki hiyo pia imesajili ukuaji wa faida kwa asilimia 184 huku sababu zilizchongia kukua ni pamoja na ukuaji wa njia za uzalishaji huku akisema kuwa amana za wateja ziliongezeka kwa asilimia 11 kutoka sh. bilioni 70 hadi bilioni 77 mwaka jana.

Katika hatua nyingine Dkt Mwangalaba alisema mwaka 2022 benki ya maendeleo imefanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa wamachinga zaidi ya 2500.

Dkt Mwangalaba alisema kwamba mwaka huu 2023 Benki hiyo inatarajia kuwafikia Wamachinga zaidi ya elfu tano,pamoja na makundi ya Wanawake na vijana kuwapatia Elimu ya biashara na kuwapatia mikopo yenye riba nafuu Kwa wale wanaokidhi vigezo ili kuweza kuwainua kiuchumi.

Hata hivyo alisema kwamba Benk hiyo inatarajia kufungua tawi jipya Mbagala Jijini Dar es salaam,kuanzisha huduma za mtandao( Internet Banking) na huduma ya ulipaji na upokeaji wa malipo ( Payment Collection System) itakayotumika Kwa ajili ya kulipa ada mashuleni pamoja na kulipa gharama za matibabu hospitalini.

” Mfumo huu unasaidia kulipa ada au malipo ya gharama za matibabu hospitalini,mfumo huu ukilipa tu taarifa zinafika sehemu husika hakuna haja ya kupeleka risiti ya malipo ,tunafanya hivi Ili kuwaondolea wazazi usumbufu wa kupeleka risiti shuleni au hospitalini,” alisema Dkt Mwangalaba.

Aidha benki hiyo imeendelea kujihimirisha katika huduma za teknolojia kwa kutambulisha thamani ya bidhaa za kidigitali ikiwemo benki mtandao, mfumo wa ukusanyaji wa malipo –PCS hatua iliyotajwa kuongeza faida kwa wanahisa kufikia zaidi ya asilimia 10.