May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya KCB yashiriki uzinduzi wa Fungua Trust

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali imesema imeandaa mipango mikakati madhubuti ya kuweza kuhakikisha sera na sheria zimekaa vizuri katika kufungua fursa zaidi kwa vijana, ikiwemo upatikanaji wa ajira hasa katika soko la Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi wakati akizindua programu mpya iitwayo The Fungua Trust, yenye lengo la kuwapa fursa au kuwajengea uwezo wahitimu wa vyuo vikuu Tanzania ili kuweza kuchangamkia fursa zinazoletwa na utangamano wa jumuhiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jana katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Programu hiyo maalumu ambayo imedhaminiwa na Benki ya KCB, ilienda sambamba na utoaji mafunzo kwa wanafunzi vijana katika Chuo hicho lengo ikiwa ni kuwasaidia kufungua macho kuona fursa zilizopo ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania hasa kutumia vizuri soko la Afrika Mashariki.

“Serikali tumeshaandaa mipango mikakati madhubuti ya kuweza kuhakikisha kwamba katika upande wa sera zimejaa vizuri katika kufungua fursa zaidi kwa vijana, sheria lakini pia kuweza kufungua uwanda, kwenye maeneo ya uwekezaji utakumbuka RAIS Dtk. Samia Suluhu Hassan tumeshafungua na kubadilisha sera na sheria za uwekezaji ili kuingiza uwekezaji mkubwa zaidi ndani na nje ya nchi lakini pia sera ya Afrika Mashariki kupitia Bunge la Afrika Mashariki”

“Soko la Afrika Mashariki Lina maeneo mengi ya nyanja za kisiasa, kiuchumia na kiutamaduni lakini limejikita zaidi katika eneo la kiuchumi.”Aliongeza Katambi

Aidha Katambi amesema serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za Benki ya KCB kupitia programu ya kutafuta vijana zaidi ya 5000 wa kuwafanyia mafunzo mbalimbali kwa kuwapeleka kwenye fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali.

“Benki ya KCB imekuwa benki kiongozi kwenye maeneo ya vijana na sasa wanaenda kwenye programu ya kutafuta vijana zaidi ya 5000 wa kuwafanyia mafunzo mbalimbali kwa kuwapeleka kwenye kuunlock potential zilizopo katika maeneo mbalimbali hivyo ni hatua kubwa na nzuri ambayo kwa niaba ya serikali tunaiunga mkono”

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo Cha Biashara Binafsi na wateja rejareja Benki ya KCB, Abdul Juma amesema wamekua wakiunga mkono masuala ya vijana ikiwemo kupitia programu ya 2Jiajiri ambayo inachukua vijana wengi wasio na ujuzi na kuwapatia mafunzo mbalimbali ya kazi za mikono, lakini pia ujuzi ambao wanaufanya wenyewe na kuwatafutia fursa ya kuajiriwa sehemu tofauti tofauti.

Kuhusu Programu ya The Fungua Trust, Juma amesema Programu hiyo ni endelevu na kila wakati vijana wakifika Benki ya KCB watakuwa waawasaidia vijana hao kuwaonyesha masoko ya Afrika Mashariki.

“Tumeshirikiana na Funguka Trust Fund ili kazi za vijana zifike katika soko la Afrika Mashariki”

Mwakilishi wa uongozi wa chuo kikuu Cha Dar es Salaam, Hezron Makumbi amesema katika Jumuhiya ya Afrika Mashariki wanajitahidi kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia na Sekta Binafsi katika kujenga uwezo wa wahitimu wetu, Kuzitambua na kuzishika fursa mbalimbali za ajira lakini pia fursa za mafunzo kwa vitendo ili waweze kupambana zaidi na kuimarika katika soko la ajira.

Aidha amewataka Vijana wahitimu kuchangamkia fursa kama hizo kwasababu jumuhiya ya Afrika Mashariki ni eneo Pana lenye soko la ajira na ujasiriamali.

Mwakilishi Mkurugenzi Mkuu wa shirika la The Fungua Trust, Ernesta Mwamaja amesema Programu hiyo imekuwa ni fursa kwa vijana hivyo ameishukuru serikali kwa mchango mkubwa walioutia kwaajili ya kupanua fursa kwa vijana katika uzalishaji uchumi nchini.

“Katika Jumuhiya kuna fursa nyingi, za kiuchumi, biashara, uzalishaji n.k ambayo bado vijana wa kitanzania hawajaweza kuchangamkia ipasavyo, hivyo tumezindua programu hii imekua ni fursa njema kwakuwa hiki ndio chuo mama kwa kuanzishwa hata kwa kazi wanazozifanya ikiwemo za kitaaluma hata za kitafiti.”

“Tunaishukuru serikali kwa mchango mkubwa ambayo inafanya kwaajili ya kupanua fursa za vijana, vijana takribani 60% ya watanzania hivyo serikali inavyofanya juhudi ya kuweka uwezo na kupata fursa ya kuongeza mchango wa vijana katika uzalishaji uchumi ni jambo la muhimu”

Naye Rais wa Serikali ya wanafunzi, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Hamisi Seif ameushukuru Uongozi wa The Fungua Trust kwa programu hiyo ambayo kwa mara ya kwanza wameweza kuifungua katika chuo Cha UDSM kwani wamejifunza mengi lakini pia amemshukuru Naibu Waziri Katambi kwa kuungana nao kuweza kuelezea ni namna gani vijana wanaweza kutumia nafasi walizonazo na muda walionao kuwekeza katika kesho zao.

“Nimekuamini nikifurshishwa na programu hii namna ambavyo inamuandaa kijana, kwa kujiamini, kuendelea kujifunza na kuziona fursa nyingi ambazo zinapatikana Afrika Mashariki”

Mwanafunzi na Rais wa Jumuhiya ya wapingwa rushwa wa chuo kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Samweli Sebastiani amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta wawezeshaji wengi chuoni hapo ambao wamejitolea kwa vijana hivyo amewataka vijana wenzake kuhakikisha wanatumia fursa hizo ipasavyo kwa kutumia akili, nguvu, vipaji na uzoefu wao ili kuweza kuingia katika soko la ajira hasa soko la Afrika Mashariki.

Isack Sumbari ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) amesema Programu hiyo itaenda kuwanufaisha moja kwa moja katika upataji wa ajira kwasababu lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanapunguza uhaba wa ajira kwa vijana hivyo alisema watatumia vyema fursa hizo na kusoma kwa bidii ili kuweza kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuingia Moja kwa moja katika program hiyo.