February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Exim yazindua suluhisho la malipo ya kisasa kwenye Z- Summit 2025

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

BENKI ya Exim Tanzania imeimarisha dhamira yake ya kukuza na kuendeleza sekta ya utalii Zanzibar kwa kushirikiana na wadau muhimu wa sekta hiyo, wakiwemo Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ili kuwezesha waendeshaji wa shughuli za utalii kufanya malipo kama ada za kuingia kwenye hifadhi kwa haraka, kwa usalama na kwa urahisi.

Mkutano wa Z-Summit 2025, uliofanyika katika Chuo Kikuu cha SUZA, Tunguu hapo Jana uliwakutanisha wadau wa Serikali, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya utalii na ukarimu ili kujadili suluhisho bunifu za kuboresha nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika mapema Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Shani Kinswaga, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, alisisitiza safari ya benki hiyo na Z-Summit tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa huu ni mwaka wa tatu mfululizo wa udhamini wao katika mkutano huo.

“Mkutano huu ni jukwaa muhimu la kushirikiana, kubadilishana maarifa na kujadili mikakati ya kuimarisha zaidi nafasi ya Zanzibar kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani na uungwaji mkono wa Benki ya Exim unaonesha imani yetu thabiti katika sekta ya utalii kama kiini cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii,” alisema Kinswaga.

Kinswaga alielezea juhudi za benki hiyo katika kutumia teknolojia kutoa suluhisho rahisi za kifedha zinazokidhi mahitaji ya biashara za utalii. kwa kuongezeka kwa mahitaji ya miamala ya kidigitali, Benki ya Exim imeanzisha huduma bunifu za kibenki, zikiwemo kutumia simu, kadi, na mifumo ya malipo mtandaoni, ili kuhakikisha ufanisi, usalama, na urahisi kwa wafanyabiashara na watalii.

Akizungumzia ushirikiano wao na TANAPA, Andrew Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha Benki ya Rejareja wa Benki ya Exim, alisema, “Katika Benki ya Exim, tunatambua kuwa ufanisi, usalama, na urahisi ni muhimu katika sekta ya utalii.

Ndiyo maana tumeshirikiana na wadau kama TANAPA na NCAA kuwezesha malipo yasiyo ya fedha taslimu kwa huduma mbalimbali, ikiwemo ada za kuingia kwenye hifadhi, akaunti ya waendeshaji wa shughuli za Utalii inajumuisha Kadi ya Exim TANAPA, iliyoundwa mahsusi kurahisisha miamala katika maeneo yote ya hifadhi nchini Tanzania.” alisema.

Katika kuthibitisha dhamira yake ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, Benki ya Exim ilitangaza mpango wake wa kuendelea kupanua huduma zake Zanzibar, Ikiwa tayari na matawi mawili yanayofanya kazi, benki hiyo ina mpango wa kufungua matawi katika maeneo mengine ya kimkakati. Hii inaonesha azma ya Benki ya Exim ya kusogeza huduma za kibenki karibu na biashara, ikiwawezesha kupata suluhisho za kifedha zinazosaidia maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa biashara, na ufanisi wa uendeshaji.

Kadri mazingira ya utalii yanavyoendelea kubadilika, Benki ya Exim inasalia kuwa mshirika wa kuaminika wa kifedha kwa biashara zinazotaka kupanuka, kuboresha huduma zao au kuwekeza katika fursa mpya.

Kupitia ushirikiano imara, matumizi ya teknolojia za kidigitali, na upanuzi wa huduma zake, Benki ya Exim haitoi tu msaada kwa sekta ya utalii bali pia inachangia katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.

Ushiriki wa Benki ya Exim katika mkutano wa Z-Summit 2025 ni uthibitisho wa dhamira yake isiyotetereka ya kusaidia ukuaji endelevu wa sekta ya utalii Zanzibar. Kwa kushirikiana na wawekezaji, wafanyabiashara, na mamlaka za serikali, benki hiyo inaunda mustakabali ambapo utalii utaendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi, kuongeza ajira, na kuifanya Zanzibar kuendelea kuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutoka kote ulimwenguni.