January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki Ya Exim Yahitismisha kampeni ya “Chanja Kijanja, Kimasta Zaidi’’ kwa mafanikio, yatangaza washindi watatu kuelekea Dubai, Uturuki na Afrika Kusini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya Exim Tanzania imehitimisha kampeni yake ya “Chanja Kijanja, Kimasta Zaidi’’ kwa mafanikio huku ikitangaza washindi wa droo kubwa ya kampeni hiyo waliojishindia safari ya mapumziko yaliyolipiwa gharama zote katika mataifa ya Dubai, Uturuki na Afrika Kusini wao pamoja na wapendwa wao.

Kampeni hiyo ya miezi mitatu ililenga kuwashawishi wateja wa benki hiyo wanaomiliki kadi za MasterCard kufanya miamala zaidi kwa kutumia kadi hizo badala ya malipo ya fedha taslimu pindi wanapohitaji kufanya malipo mbalimbali katika vituo vya mauzo (POS) au tovuti za biashara ya mtandaoni.

Washindi hao John Ren ambae ni mkazi wa Dar es Salaam, Hamza Ngilini, mkazi wa Dodoma na Ntemi Ezekiel mkazi wa Dar es Salaam walipatikana kupitia droo kubwa ya mwisho iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam mapema hii leo chini ya usisamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa washindi hao Mkuu wa Kitengo cha wateja binafsi na biashara kati wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Andrew Lyimo alisema mbali na washindi hao wa droo kuu, kupitia kampeni hiyo pia ilishuhudiwa jumla ya washindi 300 wanaotumia kadi za Exim Mastercard kufanya miamala wakijishindia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, Simu janja (Smart Phones) kila wiki na kila mwezi.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza washindi wetu wote na zaidi pia niwapongeze washindi wa droo yetu kubwa tuliyoifanya hii leo. Kufuatia ushindi huu tunatarajia kwamba washindi hawa watatu watakuwa tayari kufurahia safari ya mapumziko ya siku tano (5) wao pamoja na wapendwa wao, safari ambayo itagharamiwa kila kitu na benki ya Exim ikiwemo visa, tiketi ya ndege pamoja na pesa za matumizi.’’

“Kama tulivyobainisha hapo awali John Ren ambae ni mshindi wa kwanza ataelekea Dubai, yeye na mpendwa wake na wakiwa huko watapata fursa ya kutembelea vituo mbalimbali ikiwemo ‘Museum Of The Future’ pamoja na Jangwa la Safari. Mshindi wa pili Hanza Ngilini yeye atakwenda nchini Uturuki na mpendwa wake na wakiwa huko watapata fursa ya kutembelea vivutio kadhaa ikiwemo Msikiti maarufu wa Bluu uliopo kwenye jiji la Istanbul,’’ alisema.

Aidha Bw Lyimo aliongeza kuwa mshindi wa tatu Ntemi Ezekiel atapata fursa ya kutembelea nchi ya Afrika Kusini yeye pamoja na mpendwa wake ambapo wakiwa huko pia watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini humo.

Akizungumzia zaidi mafanikio ya kampeni hiyo Mkuu wa Idara ya Huduma Mbadala Kupitia Mifumo ya Kidigitali, Bw Silas Matoi alisema tangu kuanza kwake imefanikiwa kuvutia zaidi wateja wa benki hiyo kutumia kadi zao Exim Bank MasterCard hatua ambayo alisema inaisaidia benki hiyo kuelekea katika mapinduzi ya kihuduma yanayoendana na maboresho makubwa ya teknolojia katika utoaji wa huduma zake za kifedha.

“Ifahamike kwamba dhamira ya msingi ya benki ya Exim ni kuandaa jamii yenye utamaduni wa kutotembea na pesa taslimu na badala yake wafanye malipo kwa njia za kielektroniki hatua ambayo pia imekuwa ikipigiwa chapuo na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia katika kufanya miamala ya kifedha. Huu ndio ulikuwa msingi mkubwa wa kampeni hii tunayoihitimisha leo kwa mafanikio makubwa,’’ alisema.

Mbali na droo kubwa kampeni hiyo ilitanguliwa na droo za kila wiki ambapo wateja 15 waliobahatika walipata nafasi ya kujishindia zawadi ya fedha taslimu Tshs. 100,000/- kila wiki huku pia kila mwezi kukiwa na droo ambapo wateja walipata nafasi ya kujishindia simu janja aina ya iPhone 14 Pro mpya.

Mkuu wa Kitengo cha wateja binafsi na bishara za kati wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Andrew Lyimo (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu hitimisho la kampeni maalum ya benki hiyo inayofahamika kama “Chanja Kijanja, Kimasta Zaidi’’ iliyokuwa inalenga kuwashawishi wateja wake wanaomiliki kadi za MasterCard kufanya miamala zaidi kwa kutumia kadi hizo pindi wanapohitaji kufanya malipo mbalimbali katika vituo vya mauzo (POS) au tovuti za biashara ya mtandaoni. Tukio hilo limefanyika jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo Bw Stanley Kafu (Katikati), mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania Joram Mtafya (wa pili kushoto) na ofisa wa benki hiyo Gregory Malembeka (Kushoto).
Mkuu wa Idara ya Huduma Mbadala Kupitia Mifumo ya Kidigitali, Bw Silas Matoi (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu hitimisho la kampeni maalum ya benki hiyo inayofahamika kama “Chanja Kijanja, Kimasta Zaidi’’ iliyokuwa inalenga kuwashawishi wateja wake wanaomiliki kadi za MasterCard kufanya miamala zaidi kwa kutumia kadi hizo pindi wanapohitaji kufanya malipo mbalimbali katika vituo vya mauzo (POS) au tovuti za biashara ya mtandaoni. Tukio hilo limefanyika jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha wateja binafsi na bishara za kati wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Andrew Lyimo (katikati) na Mkuu wa Idara ya Masoko na (Kulia), Mawasiliano wa Benki hiyo Bw Stanley Kafu (kushoto).
“Chanja Kijanja, Kimasta Zaidi’’