April 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Exim yaboresha uchukuaji mikopo kwa watumishi wa umma

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar

Benki ya Exim Tanzania inajivunia kutangaza maboresho katika huduma yake ya “Wafanyakazi Loan,” ambayo sasa inajumuisha suluhisho la uchukuaji wa mikopo.

Hatua hiyo ni ya kimkakati ya kusaidia wafanyakazi wa Serikali kufikia malengo yao ya kifedha,ambapo benki hiyo imekuwa taasisi ya kwanza ya kifedha nchini, kuwezesha uchukuaji wa mikopo kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kutoka taasisi zingine kupitia mfumo wa Utumishi Portal (ESS).

Aprili 3,2025,Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na Kati kutoka Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo,amesema,”Lengo letu ni kuwapatia wafanyakazi wa Serikali huduma za kifedha zinazobadilisha maisha yao kimaendeleo. Kwa kuwachukulia mikopo yao kutoka taasisi nyingine, tunalenga kupunguza mzigo wao wa kifedha na kuwapatia masharti nafuu zaidi ya marejesho yanayolingana na mahitaji yao ya kifedha,”.

Amesema wafanyakazi wa Serikali sasa wanaweza kupata mikopo ya hadi milioni 200, yenye muda wa kurejesha hadi miaka 10 (miezi 120).Pia inawawezesha watumishi wa umma kupata mtaji wa kifedha unaowawezesha kuanzisha au kupanua biashara zao, hivyo kujiongezea vyanzo vya mapato zaidi ya mishahara yao.

“Tunatambua changamoto za kifedha zinazowakabili waajiriwa wa Serikali, na kupitia mpango huu, tunalenga kuwasaidia kupata utulivu wa kifedha,”.

Kwa upande wake Mkuu wa Bidhaa na Uhakika wa Mapato, Mtenya Cheya,amesema waombaji wa mikopo wataweza kuongeza kiwango cha mkopo wao kila baada ya miezi mitatu.

Huku marejesho ya mkopo yatakuwa katika mfumo wa Malipo Sawa ya Kila Mwezi (EMI) kwa muda wote wa mkopo, hivyo kuwawezesha wateja kupanga bajeti zao kwa urahisi.

Aidha, mkopo huo unajumuisha bima ya maisha katika kipindi cha mkopo, ambayo inahakikisha kuwa deni linalobaki litalipwa endapo mkopaji atafariki au kupata ulemavu wa kudumu,hii inatoa amani ya akili kwa mfanyakazi na familia yake.