January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB yazindua mfumo mpya wa kidijitali

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2024, Benki ya CRDB imezindua rasmi mfumo mpya wa kidijitali wa huduma kwa wateja unaotumia teknolojia ya akili mnemba (AI), iliyopewa jina la ‘Elle,’ ikiwa ni kifupisho cha ‘Ellephant’, inayowakilisha chapa ya Benki hiyo.

Uzinduzi wa mfumo huo ambao unalenga kutoa usaidizi kwa wateja kwa njia ya mawasiliano ya ujumbe ‘Chatbot’, na ufanyaji wa miamala, ulifanyika katika Makao Makuu ya Benki hiyo, ukihudhuria na zaidi ya wateja 200 wa benki hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja na mfumo huo mpya wa huduma kwa wateja, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amewahakikishia wateja kuwa huduma bora siku zote imekuwa kipaumbele cha benki hiyo, na uzinduzi wa Elle unalenga kuongeza ufanisi katika huduma za kidijitali.

“Elle inatoa majibu ya papo hapo, usahihi wa taarifa, na urahisi wa kutumia huduma zetu kupitia tovuti yetu na WhatsApp,” amesema Nsekela.

Akielezea zaidi, Nsekela amefafanua kuwa Elle itawasaidia wateja kupata majibu ya maswali au changamoto wanazozipata pindi watumiapo huduma, kufanya miamala, na kupata usaidizi wa haraka bila kuhitaji kuwasiliana moja kwa moja na wakala wa huduma kwa wateja. Pia, mfumo huu unaweza kuunganisha wateja na mawakala pale ambapo huduma za kibinafsi zinahitajika.

Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka huu inaadhimishwa kwa kaulimbiu ya “Above and Beyond,” ambayo inaendana na falsafa ya Benki ya CRDB ya kuhakikisha huduma zao zinakidhi na kuzidi matarajio ya wateja.

Nsekela amewahakikishia wateja kuwa benki hiyo itaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika teknolojia, ubunifu wa huduma na bidhaa, pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi ili kuhakikisha huduma zinazotolewa ni bora na za kiwango cha juu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Yolanda Uriyo, ameeleza kuwa benki hiyo inaendelea kuimarisha mifumo yake ya kidijitali na kuwekeza zaidi kwenye mbinu za kisasa za kupokea maoni ya wateja kupitia mifumo kama QR-Code na USSD.

“Huduma bora kwa wateja kwetu ni ajenda ya kila siku,” amesema Uriyo, akibainisha kuwa Elle ni sehemu ya mikakati ya Benki ya CRDB ya kutoa huduma za kibenki zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani. Kupata usaidizi au huduma kupitia Elle mteja anatakiwa kutembelea tovuti rasmi ya Benki ya CRDB (www.crdbbank.co.tz) au kuwasiliana kupitia WhatsApp namba (+255) 0714197700.

“Kupitia WhatsApp, Elle asaidia wateja kufanya miamala kwa urahisi ikiwamo kutuma fedha, kuangalia salio, kulipia ankara, kuangalia taarifa ya akaunti, pamoja na huduma nyengine nyingi. Mteja pia anaweza kuzungumza na ‘Elle’ kuhusu mambo mengine nje ya benki, jambo linalomfanya kuwa rafiki zaidi wa wateja,” ameongezea Yolanda.

Benki ya CRDB inatambulika ndani na nje ya kama Benki kinara katika Huduma kwa Wateja nchini.

Hivi karibuni Benki hiyo imetunukiwa Tuzo ya Ubora wa Huduma na Taasisi ya Utafiti wa Ubora barani Ulaya (European Society for Quality Research).

Kuzinduliwa kwa Elle kunaendelea kuiweka Benki ya CRDB katika ramani ya Benki kinara katika huduma bora katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Ahmed Zahoro, moja ya wateja wa Benki ya CRDB waliopata kushuhudia uzinduzi wa huduma hiyo ameipongeza benki hiyo kwa kuendeleza kuwekeza katika ubunifu kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wateja.


“Tunaishukuru Benki yetu kwa kutujali. Elle itasaidia kutupa urahisi na unafuu wa kupata huduma na usaidizi kwa wakati,” aliongeza.

Akielezea kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo amebainisha kuwa katika mwezi huu wa Oktoba, Benki ya CRDB itafanya shughuli mbalimbali ikiwamo kuwasikiliza wateja wake na kufanyia kazi maoni yao, sambamba na kuendelea kusherehekea mafanikio katika kuboresha huduma kwa wateja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wapili kushoto) akiwa pamoja na viongozi waandamizi wa Benki ya CRDB, pamoja na baadhi ya wateja wa benki hiyo wakishuhudia uzinduzi wa mfumo mpya wa kidijitali wa huduma kwa wateja unaotumia teknolojia ya akili mnemba (AI), iliyopewa jina la ‘Elle’. Mfumo huo umezinduliwa leo katika hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2024 katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es Salaam.