Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha
SPIKA wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema, pamoja na Benki ya CRDB kufanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa faida wanayopata kuisaidia jamii kwenye elimu na afya, wanatakiwa kuongeza kasi ya kutoa mikopo kwa wakulima ili waweze kulima kwa tija.
Amesema wakulima wengi nchini bado wanabahatisha, kwani wanategemea mvua ili kupata mazao yao, jambo ambalo ni hatari kama atakuwa amekopa fedha benki, huku amekopa mkopo benki, lakini kama atakuwa amewezeshwa kwa kilimo cha umwagiliaji, ataweza kukopa na kurudisha mkopo.
Ameyasema hayo leo Mei 20, 2022 kwenye semina kwa wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika jijijini Arusha, ambapo yeye alikuwa mgeni rasmi.
Dkt. Tulia amesema kilimo cha umwagiliaji kina tija kwa wakulima, lakini ili mkulima aweze kufikia hatua hiyo ni lazima awekeze, hivyo benki kama CRDB ina uwezo mkubwa wa kuweza kuwakopesha wakulima hao, na wakaweza kuinuka kutokana na kilimo chao.
“Nikisema nitaje mafanikio ya Benki ya CRDB ni mengi, lakini leo naomba nielezee changamoto zinazowakabili wakulima wetu. Wakulima wetu huko vijijini bado wana changamoto nyingi ikiwemo kilimo cha kubahatisha cha kutegemea mvua. Mkulima kama huyu ana hatari kubwa kama amechukua mkopo na mvua ikawa haikunyesha.
“Hivyo naiomba Benki ya CRDB iongeze bidii katika kuwasaidia wakulima wetu. Najua inatoa mikopo kwa wakulima wetu, lakini inatakiwa iongeze zaidi, kwani ina uwezo wa kuwekeza kwa wakulima hawa kwa kuwapa mikopo ili kuweza kulima kwa tija kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji” alisema Dkt. Tulia.
Dkt. Tulia alisema Benki ya CRDB imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo katika kutoa faida inayopata, na kupeleka huduma kwa wananchi, na wamefanya hivyo zaidi kwenye nyanja ya elimu na afya, hivyo Serikali ipo tayari kushirikiana na benki kama mdau wa maendeleo ili kuwasaidia wananchi kujikwamua kwenye masuala ya uchumi, elimu na afya.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema semina hizo zimekuwa na matokeo chanya na wamekuwa wakishuhudia ukuaji wa uwekezaji wa wanahisa, na kupelekea kuvutia wawekezaji wengi ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza ndani ya benki hiyo.
“Hili ni jambo ambalo kama benki, tunajivunia sana kwani kwa kiasi kikubwa tunasaidia kuongeza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wetu ndani na nje ya benki na kuweza kuboresha maisha yao, na ndio maana kuelekea Mkutano Mkuu wetu wa mwaka huu hapo kesho, kaulimbiu yetu inasema “Thamani Endelevu”.
“Malengo yetu ya semina hii pia nikuona Watanzania wengi wanashiriki masoko ya mitaji jambo ambalo litaongeza manufaa kwetu, makampuni mengine yanayoshiriki katika masoko ya mitaji, na Taifa letu kwa ujumla wake. Ninaposema manufaa kwa Taifa najisikia fahari kuwa sisi Benki ya CRDB ni sehemu ya taasisi ambazo serikali yetu imeweza kunufaika kwa uwekezaji ambao imeufanya” alisema Nsekela.
Nsekela alisema kwa kipindi cha mwaka 2021 Benki iliweza kukabidhi gawio la sh. bilioni 25 kwa Serikali ambalo lilikuwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 47 kutoka kwenye gawio la sh. bilioni 17 lililotolewa mwaka 2020. Jumla ya gawio lililotolewa kwa wanahisa katika mwaka 2020 lilikuwa sh. bilioni 58. Na mwaka huu wameona Bodi imekuja na pendekezo la gawio nono. Huo ni uthibitisho tosha wa faida za uwekezaji katika hisa.
“Kipekee kabisa nichukue fursa hii kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini. Kwetu sisi tunaamini matokeo ambayo tumekua tukiyapata katika biashara yetu, pamoja na mambo mengine yanachochewa sana na jitihada za Serikali katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara. Sisi kama benki tunaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kiutendaji ili kuongeza faida na hatimaye kutoa gawio kubwa zaidi kwa wanahisa wetu” alisema Nsekela.
Nsekela ametoa rai kwa Watanzania ambao bado hawajawekeza katika hisa, kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika hisa. Na kuwahimiza kuchangamkia hasa hisa za Benki ya CRDB ambayo inaendelea kufanya vyema siku hadi siku kama ambayo wamekua wakiona kupitia taarifa zao za fedha zinazotolewa kuendana na taratibu zilizopo.
“Hisa za Benki ya CRDB bado zinapatikana kwa bei nzuri sokoni na unaweza kuzipata kupitia matawi yetu yote nchini na pia kupitia kwa madalali hisa (stockbrokers) walioenea nchi nzima. Kutokana na mikakati tuliyojiwekea, naamini huu utakuwa ni uamuzi wa faida sana kwao kwani watajihakikishia gawio zuri na endelevu. Inshalaah gawio letu litaendelea kukua zaidi na kuwa gawio bora zaidi sokoni huku bei ya hisa zetu nazo zikipanda kwa kiwango kikubwa” alisema Nsekela.
Nsekela alisema Benki ya CRDB itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo Watanzania kwa kutoa huduma bora za kibenki ikwemo mikopo nafuu, ili kwa pamoja tuweze kujenga uchumi wa taifa letu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay alisema bado muamko wa wananchi kununua hisa kwenye makampuni na mashirika ni mdogo, kwani hadi sasa ni wananchi 600,000 tu ndiyo wamejitokeza kununua hisa hizo, ambapo ni kiasi kidogo ukichukulia Tanzania ina watu milioni 60.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi