January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB yapata faida ya bil. 268.2 katikati ya UVIKO 19

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha

PAMOJA na janga lililoikumba dunia la ugonjwa wa UVIKO 19, Benki ya CRDB pamoja na kampuni zake tanzu, imeweza kupata faida ya sh. bilioni 268.2 kwa mwaka 2021 ukilinganisha na mwaka 2020 ambapo walipata faida ya sh. bilioni 165.2.

Hayo yamesemwa leo Mei 21, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela kwenye taarifa yake ya mwaka aliyoisoma mbele ya Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika jijini Arusha.

“Zaidi ya hilo, tuliboresha mizania yetu kwa ukuaji mkubwa wa mikopo, kudumisha mtaji wa kutosha, na kuimarisha ufanisi na uendeshaji wetu.

Uimarishaji wa ufanisi wa uendeshaji wetu ni jambo muhimu sana kwetu kwa kuzingatia agizo la mdhibiti kuhusu uwiano wa gharama kwa mapato (CAR) mnamo Januari, 2021.”

Agizo hilo linalotaka benki kuratibu uwiano wa ufanisi hadi chini ya asilimia 55 kufikia Desemba, 2022. Tulipata uwiano wa mapato kwa asilimia 55.3 ikichangiwa na ukuaji wa mapato sambamba na mikakati ya kudhibiti gharama ambayo tulitekeleza mwaka mzima” alisema Nsekela.

Nsekela alisema kampuni tanzu ziliendelea kuchangia vyema katika biashara yao, huku biashara ya Burundi ikitoa faida ya sh. bilioni 12.8, huku kampuni tanzu ya bima ikirudisha faida ya sh. milioni 859 ikiwa ni punguzo la asilimia 76.3 kutoka mwaka 2020.

Kampuni tanzu ya Burundi inaendelea kuonesha uwezo mkubwa, ikichagizwa na uimara wa soko na kuanza kuinuka kwa uchumi baada ya janga la UVIKO 19, huku uhusiano mzuri wa Serikali ya Tanzania na Burundi ukichangia mafanikio hayo.

Alisema mwaka 2021 ulikuwa wa kipekee kwa sekta ya benki hapa nchini, na hasa Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu. Licha ya mabadiliko katika upande wa udhibiti, sekta ya benki iliendelea kuwa tulivu, ikichochewa na kuimarika taratibu kwa uchumi wa dunia.

Juhudi za makusudi za utawala wa kisiasa za kuimarisha sekta ya kibinafsi, kuongeza imani ya wawekezaji, na kuboresha mahusiano ya nje ya nchi, pia zilichangia kwa kiasi kikubwa.

“Kwa kifupi, sekta ya benki kwa ujumla ilikuwa imara, ikidumisha ukwasi wa kutosha.

Kulikuwa pia na kuendelea kwa uimarishaji wa sekta ambapo angalau benki nane (8) zilianza mchakato wa kuungana ili kukidhi mahitaji ya ukwasi kwa viwango vya mdhibiti wa sekta” alisema Nsekela.

Nsekela alisema kwa kujifunza na changamoto za mwaka 2020, walijitahidi kudumisha mahusiano ya karibu na wateja ili kuelewa hali zao na kisha kuwasaidia kurejea katika hali bora kiuchumi.

Waliendelea kuwapa wafanyakazi wao maarifa na ujuzi unaohitajika ili kusaidia ipasavyo wateja wao wakati huo. Pia kutoa masuluhisho mapya ambayo yaliundwa kukidhi mahitaji ya soko.

Alisema katika kudumisha shughuli za kimkakati, mafanikio mengi ya mwaka 2021 ni zao la ushirikiano wa karibu wa wadau wao ikiwa ni pamoja na mdhibiti, washirika wa kibiashara na wateja. Wanaelewa kuwa kushirikisha wadau mara kwa mara na kwa uwajibikaji, kuna matokeo chanya kwa biashara yao katika kipindi cha muda mfupi na mrefu.

“Katika mwaka wa fedha wa 2021 tuliyafikia makundi tofauti ya wadau, na kuwahusisha kwa namna mbalimbali kuhusu masuala muhimu, ambayo mengi yana uhusiano wa moja kwa moja kwenye biashara yetu. Jambo lililotia fora ilikuwa ni ziara ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kampuni yetu tanzu ya Burundi mjini Bujumbura, wakati wa ziara yake ya kwanza ya kiserikalini nchini humo katikati ya mwezi Julai.”

“Mashirikiano mengine muhimu ni pamoja na kushiriki katika Kongamano la Hali ya Hewa la Umoja wa Mataifa (COP 26) huko Glasgow, Uingereza kama sehemu ya jitihada zinazoendelea kwa Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu kuwa bingwa wa masuala endelevu katika utunzaji wa mazingira.

Pia, tulikuwa na ziara ya kibiashara yenye mafanikio nchini Italia, ambapo tulifadhili baadhi ya wateja wa makampuni kuhudhuria kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania katika sherehe za miaka 60 ya Uhuru iliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa” alisema Nsekela.

Nsekela alisema mwaka wa fedha 2022 ni wa mwisho wa mkakati wao wa muda wa kati na kama inavyotajwa, ni lazima wafanye tathmini ya kile ambacho wameweza kufanikiwa katika kipindi chote cha mkakati.

Kipaumbele chao ni kuimarisha vichochezi vya ukuaji wa kujenga msingi imara kwa ajili ya mafanikio endelevu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay alisema kama Benki ya CRDB na kampuni tanzu zake, uendeshaji wao benki ni endelevu, na unatokana na uwezo wao wa kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji. Na wana mkakati kabambe wa upanuzi wa utoaji huduma za kibenki kwenye soko la Afrika Mashariki na Kati.

“Tunataka kuwa vinara wa ubunifu ambao utabadili mfumo wa sekta ya fedha katika miaka ijayo. Masoko mapya yenye jumla ya watu milioni 500 yatatoa changamoto mtambuka na mahitaji mbalimbali ambayo tunataka kutengeneza masuluhisho yake. Mafanikio ya kampuni yetu ya kampuni tanzu ya Burundi, haswa katika kuimarisha biashara baina ya nchi, yanaendelea kutupa hamasa ya kukuza wigo wetu wa utoaji huduma.”

Kufuatia taarifa ya mwisho kuhusu kuingia kwetu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), nafurahi kuripoti kwenu kwamba tumepata maendeleo makubwa katika kupata leseni na vibali vinavyohitajika kutoka kwa mamlaka za nyumbani pamoja na DRC. Tunatarajia kuanza uendeshaji ndani ya nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2022″ alisema Dkt. Laay.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ambao unaendelea leo Mei 21, 2022 kwenye Ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB unaofanyika leo Mei 21, 2022 kwenye Ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ukiendelea leo Mei 21, 2022 kwenye Ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ukiendelea leo Mei 21, 2022 kwenye Ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ukiendelea leo Mei 21, 2022 kwenye Ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ukiendelea leo Mei 21, 2022 kwenye Ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ukiendelea leo Mei 21, 2022 kwenye Ukumbi wa Simba, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.