January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki, taasisi za kifedha zahimizwa kuwekeza katika sekta ya uvuvi nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

BENKI na taasisi za kifedha Nchini zimehimizwa kuikopesha mitaji miradi ya sekta ya uvuvi ili kuchochea uzalishaji wa mazao ya uvuvi na kuchangia kuinua uchumi.

Akieleza matarajio yake baada ya kutembelea Makao Makuu ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia uvuvi, Dkt. Rashid Tamatama, amesema kuwa sekta ya uvuvi ina nafasi kubwa ya kutengeneza ajira kwa vijana, kwani mahitaji ni mkubwa kulinganisha na uzalishaji wa mazao ya uvuvi.

Mahitaji ya mazao ya uvuvi ni tani 750,000 kwa mwaka, lakini mavuno kwa sasa ni tani 483,000 tu. Amesema kuna pengo kubwa kufikia mahitaji na kufafanua kwamba pengo hilo ni fursa kwa taasisi za fedha kuchochea uwekezaji katika sekta hiyo ili kuzalisha ajira.

Ameeleza kuwa jiografia ya Tanzania inaruhusu kufanya shughuli za uvuvi kwani ina eneo kubwa la bahari, maziwa na mito. Amesema maeneo hayo yakitumiwa inavyostahili taifa litapiga hatua kubwa ya uzalishaji katika sekta hii na kuifanya itoe mchango mkuba zaid katika pato la taifa.

TADB ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza na kukuza sekta za kilimo,mifugo na uvuvi, hivyo benki hiyo ihamasishe benki nyingine za kibiashara ili mitaji ipatikane na uwekezaji ufanywe kwenye sekta hii, amesema Dkt.Tamatama

ufugaji samaki

Ameeleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili wavuvi wengi ni upatikanaji wa vifaa vya kufanya uvuvi wa kisasa na endelevu, na kuziomba benki na taasisi za kifedha kuwekeza nguvu kwenye uvuvi ili kuongeza uvunaji wa samaki nchini.

Lengo kubwa ni kuifanya sekta ya uvuvi kuchangia katika kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuzalisha samaki kwa wingi kufikia mahitaji ya nchi na ziada kuuzwa nje ya nchi, amesema Dkt.Tamatama

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema benki yake inaunga mkono juhudi za serikali katika kuendelea sekta ya uvuvi nchini na kwamba ni busara wavuvi wakapewa mikopo ili kukuza uzalishaji.

“Sekta ya uvuvi inaajiri watu wengi, hivyo kuboresha mazingira ya uvuvi kutakuza kipato cha wananchi wengi ambao wanategemea sekta hii,” amesema Nyabundege

Amesema kupitia bajeti ya mwaka 2021/2022 serikali imeitengea TADB fedha kwa lengo la kukuza na kuendelea sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kueleza kwamba kwa sababu hiyo benki itaendelea kutekeleza wajibu wake na kuhakikisha sekta ya uvuvi inapata msukumo mpya ili kuongeza uzalishaji.

Bajeti ya Wizara Mifugo na Uvuvi ya mwaka huu wa 2021/2022 inaeonyesha kuwa watu 225,000 wameajiriwa na sekta ya uvuvi na watu zaidi ya milioni 4.5 wanapata kipato kupitia shughuli za uvuvi.