November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Beng’i: Watanzania wengi hawana elimu ya matumizi fedha za Mkopo

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

BARAZA la Taifa la uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limesema kuwa watanzania wengi bado hawana elimu ya kutosha juu  ya matumizi ya fedha itokanayo na mikopo na badala yake wanakopa bila kuwa na mipango waliyokusudia.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 14,2023 na Katibu Mtendaji wa  NEEC,Beng’i Issa wakati akizungumz na  waandishi wa habari katika kuhusu a utekelezaji wa majukumu ya Baraza hilo.

Beng’i ameeleza kuwa pamoja  na Serikali  kutoa fedha za mikopo kiasi cha shilingi Trilioni 5.6 kwa ajili ya kuwawezesha watanzania milioni 8  bado watanzania wengi wanakabiliwa nakutokua na  elimu juu ya matumizi ya fedha na kumiliki fedha.

“Nataka kuwaeleza kuwa katika kipindi cha mwaka jana baraza kwa kushirikiana na serikali kwa ujumla wake wametoa kiasi cha sh.tirion 5 .6 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wapatao milioni 8 jambo ambalo ni hatua kubwa katika kuwawezesha watanzania kujiinua kiuchumi” ameeleza Beng’i.

Kutokana na kutokuwepo kwa elimu ya kutosha juu ya matumizi ya fedha na kumiliki fedha amesema kuwa serikali kwa kushirikiana taasisi mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu juu ya matumizi ya fedha na kumiliki fedha.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa watanzania ili kuhakikisha watanzania wanajikwamua katika maisha  na kuishi maisha ambayo yatakuwa bora kila mmoja jambo ambalo litawafanya watanzania kuwa na amani na furaha” amesema Beng’i.

Pamoja na hayo Beng’i  amewashauri watanzania kutopenda  kujitumbukiza kwenye masuala ya mikopo kama hawajajipanga kwa kujua wanachotakiwa kukifanya.

Aidha amewataka watanzania  kuwa  na nidhamu ya fedha sambamba na kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba  benki.

Vilevile amezungumzia ufanisi wa baraza hilo ambapo amesema kuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanawawezesha wananchi kupata fursa mbalimbali za kujikwamua kihuchumi .

Katika kutilia mkazo juu ya kuwawezesha wananchi ameeleza kuwa kwa sasa kuna mifuko mbalimbali ya kuwawezesha akina mama na vijana huku akieleza kuwa akina mama wamekuwa wakipewa kipaumbele zaidi kwa kuwa ni waaminifu katika kurejesha.