Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Bei za rejareja za mafuta kwa mwezi Novemba 2024, zimeendelea kushuka.Ambapo bei ya petroli kwa Dar es Salaam na Tanga imeshuka kwa asilimia 2.26 ambayo ni sawa na shilingi 68 kwa lita, huku Mtwara ikiwa imepungua kwa asilimia 2.16, ikilinganishwa na bei za mafuta za Oktoba 2024.
Aidha, bei ya dizeli pia imepungua kwa asilimia 0.07 kwa Dar es Salaam, asilimia 0.17 kwa Tanga na asilimia 0.11 kwa Mtwara.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Novemba 6, 2024, imeeleza kuwa ahueni hiyo kwa bei za mwezi huu, inatokakana na kushuka kwa gharama za kuagiza mafuta ya petroli kwa wastani wa asilimia 3.91na kupungua kwa
gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa wastani wa asilimia 1.75.
Kutokana na punguzo hilo, petroli Mkoa wa Dar es Salaam itauzwa kwa shilingi 2,943 kwa lita, Tanga shilingi 2,948 na Mtwara shilingi 3,015. Kwa upande wa dizeli, bei za rejareja kwa Novemba 2024, Dar es Salaam ni shilingi 2,844 kwa lita, Tanga shilingi 2,855 na Mtwara shilingi 2,916. Mafuta ya taa yatauzwa shilingi 2,943 Dar es Salaam, shilingi 2,989, Tanga na shilingi 3,016 Mtwara.
Ikumbukwe kuwa, bei za bidhaa za mafuta aina ya petroli zimeshuka mfululizo kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Septemba 2024.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba