November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Beach Soccer waenda Senegal na matumaini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WACHEZAJI 14 pamoja na viongozi wa benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni ‘Beach Soccer’ wameondoka hapa nchini leo alfajiri kuelekea nchini Senegal tayari kwa michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (BSAFCON 2021) zitakazoanza kutimua vumbi Mei 23 hadi 29.

Nyota watakaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo ni makipa Ahmed Juma, Adam Oseja na Dhabani Kado wakisaidiwa na mabeki Eric Manyama, Rolland Msonjo, Ismail Gambo Saidi Moradi na Daniel Mwainyekule.

Wengine ni Kashiru Said, Jaruph Juma, Yahya said Tumbo, Abdulkadir ali Tabib, Ahmad Abdi Ahmad na Stephano Wallece Mapunda.

Katika michuano hiyo Tanzania imepangwa Kundi A pamoja na wenyeji Senegal, Uganda huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikitangaza kujiondoa kwenye mashindano hayo wakati kundi B likiundwa na timu ya Egypt, Mozambique, Morocco na Seychelles.

Baada ya Congo kujiondoa sasa Tanzania itatupa karata yake ya kwanza dhidi ya majirani zao Uganda Mei 24 kisha Mei 26 watakutana na Senegali amabo watakutana na Uganda katika mchezo wa kwanza utakaochezwa Mei 23.

Akizungumzia matarajio yake katika mashindano hayo, kocha mkuu wa timu hiyo, Boniface Pawasa amesema kuwa, kiufundi kikosi chao kinaondoka huku kikiwa vizuri na wana imani kubwa ya kwenda kufanya vizuri kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

Amesema wana imani kubwa na ubora wa kikosi chao cha nyota 14 wanaoondoka nao kwani licha ya kutopata mechi nyingi za kirafiki za kutosha hasa za kimataifa lakini bado wameweza kuonesha ubora wa hali ya juu.

“Tumepata mechi za ndani za kirafiki na imekuwa ngumu kupata zile za kimataifa lakini licha ya hayo tumeitumia mechi yetu dhidi ya Burundi pamoja na zile za Zanzibar kutatua mapungufu tuliyoyaona hivyo hadi sasa hari ya wachezaji ipo juu na sasa tupo katika maandalizi ya mwisho kabisa kabla ya kuanza safari yetu ya Senegal,” amesema Pawasa.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Deo Lucas amesema kuwa, baada ya kuwepo na madabiliko ya ratiba, watahakikisha wanasoma mbinu za wapinzani wao Uganda ambao watacheza mechi ya ufunguzi ya Kundi A dhidi ya Senegal.

“Naweza kusema kuwa tuna bahati sana kwani mechi yetu ya kwanza itakuwa dhidi ya Uganda ambao watacheza na Senegal watakaokutana nao katika mchezo wa pili na mwisho kwa kundi letu A jambo linalotupa matumaini zaidi ya kufanya vizuri,” amesema kocha huyo.

Itakumbukwa kuwa hii ni mara ya pili mfululizo Tanzania inafuzu kucheza fainali hizo baada ya mwaka 2018 kufanikiwa kufanya vizuri baada ya kudika nafasi ya nane katika ya nchi 52 katika viwango vya Afrika na dunia.

Tanzania ilifanikiwa kufuzu fainali hizo baada ya kupata ushindi wa jumla wa goli 12-9 wakifanikiwa kushinda goli 8-3 katika mchezo wa kwanza na kufungwa goli 6-4 katika mchezo wa marudiano uliochezwa Aprili 3 kwenye fukwe za Coco.