Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
CHAMA cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kimetengua maamuzi yake ya kuwafungia nyota saba wa mchezo huo kushiriki Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuzitumikia timu nyingine katika michuano ya CRDB Taifa Cup iliyomalizika mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma kwa timu ya Mbeya kutwaa ubingwa kwa upande wa wanaume na Temeke kwa upande wa wanawake.
Wachezaji waliotangaza kufungiwa ni pamoja na Jimy Brown (JKT) aliyechukua zawadi ya ‘Best Defender’, Baraka Sadick(JKT) aliyekuwa MVP, Musa Chacha (JKT), Isaya Aswile (Kurasini), Mwalimu Heri (Kurasini), Henrico Augustino(ABC)
na Jackson Brown (JKT).
Katika barua iliyotolewa Novemba 23 na Daniel Kapongo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa BD na nakala kupelekwa kwa viongozi mbalimbali wa klabu hizo, imeweka wazi kuwa wachezaji hao watafungiwa kucheza mashindano hayo hadi Novemba 23, 2022.
Barua hiyo imesema, klabu zote za Dar es Salaam ni wanachama wa Chama cha Mkoa ambae ndio msimamizi na muandaaji wa programu na mipango yote endelevu ya mchezo wa mpira wa kikapu, ikiwa ni pamoja na kushiriki mashindano mbali mbali ya kitaifa na kimataifa kutokea kwenye ligi hiyo hivyo kitendo cha wachezaji na viongozi wa klabu kupuuza dhamana waliopewa kuunda timu ya Mkoa na kushiriki mashindano na Mikoa mingine ambayo haina programu zozote wala ligi bila taarifa yoyote sio kitendo cha kiungwana na hakikubaliki kwani kinachokwamisha na kurudisha nyuma mipango/mikakati ya mafanikio katika mchezo wa mpira wa kikapu ndani ya Mkoa.
“Maamuzi haya yamekusudia kutoa fundisho kwa wachezaji wote ambao hawathamini jitihada zinazofanyika katika Mkoa wao na pia ni kuwapa fursa waende kuchezea Ligi za Mikoa hiyo wanayoithamini ili tuweze kujenga wachezaji wapya wazalendo, wenye nidhamu na wanaoaminika kwa ajili ya mashindano yajayo,” imeleza barua hiyo.
Pia walisema, wanaamini wachezaji hao ni matunda ya ubora na mazingira ya Ligi ambayo wadau wote wa Dar es Salaam wamekuwa wakipambana hali na mali katika kuhakikisha wanakuwa na ligi yenye ubora na viwango vya juu ukilinganisha na Mikoa yote Tanzania hivyo kitendo cha wachezaji hao kutotoa ushirikiano kwa Mkoa kitaifa ni hujuma na usaliti mkubwa.
Akitolea ufafanuzi wa hukumu iliyotolewa na BD, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Mboka Mwambusi ameuambia Mtandao huu kuwa, baada ya BD kutoa taarifa hiyo waliwasiliana nao kuwaeleza kuwa kilichofanywa na wachezaji hao hakikua kinyume na Kanuni kwani moja ya sheria ambazo zilikuwa katika mashindano ya CRDB Taifa Cup ni kuruhusu wachezaji wanne kwa kila timu kujiunga na timu za Mikoa mingine.
Hivyo baada ya taarifa hiyo kutoka, walifanya mazungumzo na kuwaeleza kile kilichopo pamoja na kanuni hiyo na waliwaelewa jambo ambalo pia liliwafanya kufikia maamuzi ya kutengua adhabu hiyo.
“Baada ya taarifa ile kutoka haraka sana tuliwasiliana na viongozi wa BD na kuwaeleza kilichofanyika hakikuwa kinyume na kanuni na ndio maana waliruhusu wachezaji wanne kwa kila timu kujiunga na Mikoa mingine na ndio maana hata mikoa mingine haikulalamika wachezaji wao wazitumikia timu nyingine,”.
“Jambo kubwa ni kuwa tunashukuru mazungumzo yetu yalikwenda vizuri kwani tayari wachezaji hao wameshafutiwa adhabu hiyo na tunaamini kama ilivyo malengo yetu wataendelea na majukumu yao kama kawaida,” alisema Mboka.
Pia amesema, watakaa kujadili baadhi ya kanuni nyingine ili kuweka mambo sawa na kuzuia lisitokee katika siku za mbeleni kwani wadhamini wa Taifa Cup, benki ya CRDB wataendelea kudhamini mashindano hayo huku wakiahidi kuyaboresha zaidi katika msimu ujao.
Kupitia mashindano hayo, CRDB walitoa Sh. milioni 50 kugharamia mafunzo ya wanakikapu vijana 24 walio na umri chini ya miaka 19 ambao wanahitaji kujiendeleza kielimu na wana sifa za kujiunga na vyuo vya ufundi stadi nchini (VETA).
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM