Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dodoma
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, amewaagiza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), kutumia fursa ya uwepo wao katika baraza hilo kuhoji na kutoa mapendekezo yatakayokuwa na mchango chanya katika kuiletea nchi maendeleo.
Huku akiipongeza Menejimenti ya Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kutekeleza takwa la kisheria na kuhakikisha Baraza la Wafanyakazi wa Bodi hiyo linaanzishwa.
Ameyasema hayo jijini Dodoma leo wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara pamoja na Mfumo wa Kieletroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini unaoziwezesha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kuwasilisha taarifa za kiutendaji kupitia mfumo huo.
“Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu mahala pa kazi linalotumika kama kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi….,kupitia baraza hili wafanyakazi na menejimenti mnapata fursa ya kujadili kwa pamoja masuala ya msingi ya taasisi ikiwemo mipango, bajeti na masuala mengine ya kiutendaji na kiutawala,”amesema Bashungwa.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga, amesema kuwa Mabaraza ya Wafanyakazi yanaanzishwa kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi kuhusu usimamizi wa rasilimali watu.
Pamoja na utekelezaji wa majukumu,kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi,maslahi ya wanyakazi na kusimamia haki na ustawi sehemu za kazi.
“Wajibu wa mabaraza haya, kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuleta matokeo ya utendaji kazi wenye tija,”amesema Kalimbaga.
Sambamba na Uzinduzi wa baraza hilo, Waziri Bashungwa amezindua pia Mfumo wa Kielektronikia wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Ujenzi, ambapo katika taarifa yake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour ameeleza kuwa Wizara pamoja na Taasisi zake wataanza kutumia rasmi mfumo huo ifikapo mwezi Mei, 2024.
“Ni matarajio ya Wizara kuwa mfumo huu utaongeza ufanisi kwa Wizara na Taasisi zake na kupunguza matumizi ya fedha za Serikali lakini pia kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi kati ya Wizara na Taasisi zake”, amesema Balozi Aisha.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato