May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bashungwa:Tumieni mabaraza ya wafanyakazi kuiletea nchi maendeleo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dodoma

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, amewaagiza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), kutumia fursa ya uwepo wao katika baraza hilo kuhoji na kutoa mapendekezo yatakayokuwa na mchango chanya katika kuiletea nchi maendeleo.

Huku akiipongeza Menejimenti ya Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kutekeleza takwa la kisheria na kuhakikisha Baraza la Wafanyakazi wa Bodi hiyo linaanzishwa.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akimsikiliza Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi hiyo uliofanyika jijini Dodoma

Ameyasema hayo jijini Dodoma leo wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara pamoja na Mfumo wa Kieletroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini unaoziwezesha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kuwasilisha taarifa za kiutendaji kupitia mfumo huo.

“Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu mahala pa kazi linalotumika kama kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi….,kupitia baraza hili wafanyakazi na menejimenti mnapata fursa ya kujadili kwa pamoja masuala ya msingi ya taasisi ikiwemo mipango, bajeti na masuala mengine ya kiutendaji na kiutawala,”amesema Bashungwa.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa (wa pili kushoto), akiimba wimbo wa wafanyakazi wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara uliofanyika jijini Dodoma,wa pili kulia ni Balozi Mhandisi Aisha Amour Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Rashid Kalimbaga Kaimu Mtendaji Mkuu Mfuko wa Barabara na Hindu Mussa Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara.

Awali Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga, amesema kuwa Mabaraza ya Wafanyakazi yanaanzishwa kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi kuhusu usimamizi wa rasilimali watu.

Pamoja na utekelezaji wa majukumu,kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi,maslahi ya wanyakazi na kusimamia haki na ustawi sehemu za kazi.

“Wajibu wa mabaraza haya, kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuleta matokeo ya utendaji kazi wenye tija,”amesema Kalimbaga.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa (Mb), akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, baada ya kulizindua baraza hilo jijini Dodoma.

Sambamba na Uzinduzi wa baraza hilo, Waziri Bashungwa amezindua pia Mfumo wa Kielektronikia wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Ujenzi, ambapo katika taarifa yake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour ameeleza kuwa Wizara pamoja na Taasisi zake wataanza kutumia rasmi mfumo huo ifikapo mwezi Mei, 2024.

“Ni matarajio ya Wizara kuwa mfumo huu utaongeza ufanisi kwa Wizara na Taasisi zake na kupunguza matumizi ya fedha za Serikali lakini pia kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi kati ya Wizara na Taasisi zake”, amesema Balozi Aisha.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara pamoja na Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini unaotumiwa na Wizara ya Ujenzi na Taasisi zake uliofanyika jijini Dodoma.