Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Kigoma
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa uchunguzi umebaini mpasuko wa ardhi na kuporomoka kwa tuta la barabara uliojitokeza katika eneo la Busunzu lenye urefu wa mita 200 haijatokana na makosa ya Mkandarasi kwenye ujenzi bali umesababishwa na sababu za kigeolojia.
Amebainisha kuwa kipande cha barabara hiyo kipo katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Manyovu – Kasulu – Kibondo – Kabingo Awamu ya tatu ya barabara ya Mvugwe hadi Makutano ya Nduta (km 59.35) ambayo ilikwishakamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
Bashungwa ametoa taarifa hiyo mkoani Kigoma Julai 10, 2024 mara baada ya kukagua eneo hilo na kupokea taarifa ya uchunguzi iliyofanywa na wataalamu wa miamba kutoka taasisi ya Geolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Kitengo maalum cha Utafiti cha TANROADS, na School of Mines and Geosciences (SoMG) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Nimepokea taarifa za kitaalamu na nimejionea zaidi ya mita 200 namna ambavyo majanga ya asili yaliyoathiri eneo hili, Serikali iliunda jopo la kufanya utafiti wa kina kuanzia Februari na tulichokigundua hapa sio makosa ya Mhandisi, sio upigaji kama watu wengine walivyodhani,”amesema Bashungwa.
Bashungwa ameitaka TANROADS kuendelea kutekeleza ushauri uliotolewa na Wataalamu hao waliofanya uchunguzi huku akielekeza kuhakikikisha wanafanya usanifu wa barabara kwenye maeneo korofi wakati wa mvua kwa kushirikiana na Wataalamu wa Miamba ili kubaini tabia za maeneo hayo na kuepuka changamoto zinazojitokeza.
Vilevile, Bashungwa ametaja miradi ya kijamii (CSR) iliyopo sehemu ya mradi huo katika Wilaya ya Kibondo ikiwa ni ujenzi wa kituo cha Afya, ujenzi wa kilometa moja ya lami, ujenzi wa shule na ujenzi wa miundombinu ya maji kwa wananchi wa Wilaya hiyo.
Bashungwa amempongeza Meneja wa TANROADS mykoa wa Kigoma kwa kusimamia Wahandisi Washauri katika miradi yote ya ujenzi ya barabara na madaraja inayoendelea kutekelezwa.
Ambapo amemtaka Mtendaji Mkuu wa TANRAODS kuhakikisha kwenye mikataba yote mipya ya barabara kuwe na kipengele cha kuwapa nguvu Mameneja wa TANROADS wa mikoa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amemueleza Waziri Bashungwa kuwa baada ya utafiti huo kufanyika hivi sasa Mhandisi Mshauri anaandaa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utakaotoa michoro na gharama za matengenezo.
Mhandisi Besta ameeleza kuwa baada ya taarifa za Wataalamu wa miamba wameshauri kurudisha barabara sehemu ile ile iliyokuwa imejengwa awali ikiwa ni pamoja kujenga upya tuta la barabara la mita 270 pamoja na kujenga surface na subsurface drainage ili kuruhusu maji yapite bila kuathiri tuta la barabara.
Naye, Diwani wa Kata ya Busunzu Wilayani Kibondo, Paul Ngomagi amemueleza Waziri Bashungwa kuwa hapo awali wananchi walikuwa wanaitumia barabara hiyo katika shughuli zao za kila siku.
Ambapo walikuwa wakitumia dakika 45 kutokea Busunzu hadi Kibondo Mjini lakini baada ya kutokea changamoto hiyo wananchi wamekuwa wakisubiria hatua za Serikali zitakazochukuliwa kurekebisha eneo hilo lililoporomoka.
Itakumbukwa mnamo Februari, 2024 mkoani Kigoma katika mradi wa barabara ya Mvugwe – Makutano ya Nduta palijitokeza nyufa ndogondogo na baadae kipande cha barabara hiyo kuongezeka kutoka mita 50 hadi kufikia mita 200 na kuporomoka chini kına cha mita 15 kutoka usawa ilipojengwa awali.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi