Na Penina Malundo,timesmajira, Online
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa  amefungua mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa huku akitoa maagizo nane kuhakikisha wanayatekeleza katika sehemu zao za kazi na kukusanya mapato mengi katika Halmashauri zao.
Miongoni mwa maagizo hayo ni pamoja kuhakikisha Wakurugenzi wa Halmashauri wanawalipa wakusanya mapato posho zao kwa wakati na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinakwenda benki kwa wakati na kuondoa mianya yote ya upotevu wa mapato ikiwemo Watumishi kushirikiana na Wakusanya Mapato kufanya udanganyifu.Â
Akitoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo hayo ya Wakuu wa Mikoa walioapishwa Juzi na Makatibu Tawala wa Mikoa,alisema ni vema kuhakikisha wanatekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sherehe za kuapishwa kwa viongozi kuhakikisha mianya ya upotevu wa mapato inazibwa.
Amesema yeyote anayecheza na mifumo ya ukusanyaji mapato achukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria na si vinginevyo.”Tuhakikishe tunatekeleza maelekezo ya Rais Samia kuhakikisha tunaziba mianya yote ya upotevu wa mapato katika Halmashauri zetu,tukiziba matobo yote kwenye pipa na kuziba mianya yote tutaona pipa linajaa hivyo tuzibe mianya hii ya upotevu wa fedha,”amesema na kuongeza.
“Hakikisheni Halmashauri zilizopo kwenye Mikoa yenu zinahuisha Leseni za Biashara ili kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani,”amesema.
Bashungwa amesema zipo baadhi ya Halmashauri mfano halmashauri za Wilaya za Kilosa na Kiteto ambazo kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka 2020/21,Halmashauri hizo hazikuhuisha leseni zao za Biashara hali iliyosababisha zikakosa mapato.
Amesema mara nyingi halmashauri nyingi uwa hazihuishi leseni zao katika upatikanaji wa mapato na kusababisha mapato kutopatikana.”Hakikisheni makisio ya bajeti za mapato ya ndani ya Halmashauri zinazingatia uhalisia wa vyanzo vya mapato ili kuwa na matokeo halisi,”amesema.
Akitolea mfano kwa baadhi ya taarifa,Bashungwa amesema  zipo halmashauri ambazo zimekusanya zaidi ya asilimia 100 lakini hazikuwahi kuomba kuhuisha bajeti zao ili ziendane na uhalisia kama vile halmashauri za Wilaya za Kibaha, Mlele na Halmashauri ya Mji wa Mbulu.Â
Amesema pia zipo Halmashauri ziliomba kupunguza bajeti zao hata hivyo, mwisho wa mwaka zimekusanya zaidi ya asilimia 100 kama vile Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti. “zipo Halmashauri ambazo zimeomba kuongeza bajeti zaidi ya mara moja katika mkwa kama vile Halmashauri za Wilaya za Morogoro, Rufiji, Kaliua na Nyang’hwale hata hivyo bado zimekusanya zaidi ya asilimia 100,hali hili inaashiria kwamba Halmashauri bado zina fursa ya kukusanya Mapato isipokuwa haziko makini katika kuchambua uhalisia wa kila chanzo ili kupata makisio halisi na hivyo kuamua kuweka kiasi chochote wanachofikiria,”amesema
Aidha Bashungwa amesema halmashauri zinatakiwa kuhakikisha  fedha zilizovuka mwaka wa fedha 2021/22 (Bakaa) zinatumika kabla au ifikapo Septemba 30, 2022 kwa kufuata Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo. “Naelekeza Halmashauri zote zenye Bakaa ziwasilishe orodha ya miradi itakayotekelezwa kwa fedha hizo kupitia Mikoa na ufanyike ufuatiliaji wa fedha hizo na kunipa taarifa ambayo nitaitoa kwa Wananchi wakati nitakaposoma taarifa ya robo ya kwanza mwaka 2022/23,”AmesemaÂ
Amesema Halmashauri zote zitekeleze mapendekezo na kufunga hoja zote za ukaguzi zilizotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) huku Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ambapo kule kumekuwepo na hoja nyingi ambazo hazijafungwa na hoja hizo zimekuwa zikijirudia pia kwenye hoja za CAG.Â
“Nataka muhakikisha Halmashauri ambazo hazikufanikiwa kukamilisha utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi yaliyotolewa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 zinakamilisha maagizo hayo kabla au ifikapo Septemba 30,2022 na kutoa taarifa Ofisi ya Rais – TAMISEMI na  kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye ngazi za Kata na kuthibiti matumizi mabaya ya fedha zinazotoka Serikali kuu na fedha za mapato ya ndani zinazoelekezwa kwenye ngazi ya Kata ili kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa kwenye miradi yenye tija kwa Wananchi,”amesema.
Pia amesisitiza kuwa Wakuu hao wanapaswa kuhakikisha ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri unajumuisha ukaguzi wa Miradi inayotokana na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu na kubainisha kiasi chote cha fedha za mikopo ya asilimia 10 ambacho hakijarejeshwa na kusimamia urejeshaji na kuwasilisha taarifa Ofisi ya Rais – TAMISEMI.Â
“Ninaelekeza mkazisimamie Halmashauri zote na kuhakikisha vikundi vyote vilivyowahi kupata Mikopo na havijamaliza marejesho vinaingizwa kwenye Mfumo na kazi ya kuingiza taarifa za vikundi hivyo iwe imekamilika ifikapo Agosti 30, 2022 na nimemuagiza Katibu Mkuu atasimamia hili kuanzia Agosti mosi kuona ni Halmashauri zipi zinatekeleza na ambazo hazifanyi chochote tutachukua hatua kwa kuwa tutakuwa na uwezo wa kuona kupitia kwenye Mfumo,” amesema na kuongeza.
“Watakwimu katika Halmashauri na Mikoa watumike ipasavyo kwani serikali haitavumilia kuona bado kuna fedha zisizorejeshwa au mikopo kutolewa kwa vikundi hewa au wanufaika wasiostahili. Ninapenda kusisitiza tena, Wakuu wa Mikoa hakikisheni mikopo yote inarejeshwa. Tufuate mfano wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika kusimamia fedha za Mikopo,”amesemaÂ
More Stories
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania
REA yajitosa kwenye nishati safi ya kupikia
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume