Na Walimu Nchini
MHESHIMIWA Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awali ya yote tunakusalimu sana na kukupa pole na pongezi nyingi sana kwa utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kulijenga Taifa letu pendwa la Tanzania,hongera sana kwa kazi nzuri inayoifanya kwa maendeleo ya Watanzania.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi ni chama cha walimu wa shule za binafsi Tanzania (TPTU-Tanzania Private Schools’ Teachers Union) , chama hiki kilianzishwa Mei 21, 2016 na kilisajiliwa rasmi serikalini Machi 28, 2018 na msajili wa vyama vya wafanyakazi na waajiri,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu
Makao makuu ya chama hiki kitaifa kwa sasa yapo jijini Mwanza,dhumuni kuu la chama hiki ni kuwaunganisha walimu wote wa shule za binafsi nchini wapatao 89,475 kuanzia walimu wa shule za awali,msingi na sekondari kuwa wamoja na wenye mshikamano katika masuala mbalimbali ikiwemo uwajibikaji mahali pa kazi,maslahi yao na kudumisha amani na mshikamano miongoni mwao na waajiri wao ili kuleta tija kubwa katika eneo la kazi.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,tumelazimika kukuandikia barua ya wazi tukikuomba sana utusaidie kutatua tatizo la mishahara yetu lililosababishwa na mlipuko wa janga la ugonjwa wa Corona, ambalo tunatambua sote na Dunia nzima inajua juu ya janga hili na madhara yake.
Hapa nchini kwetu ugonjwa huu uliingia mwezi Machi na tarehe 17-18, Machi, mwaka huu serikali ilifunga shule na vyuo kama jitihada za kujikinga na ugonjwa huu.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,mara baada ya shule kufungwa hapa nchini waajiri wa shule za binafsi walianza kusitisha mikataba,kutoa barua za likizo bila malipo na kutolipa kabisa mishahara kwa walimu wao kwa hoja ya kuwa shule kufungwa na kukosa chanzo cha mapato ambazo ni ada za wanafunzi.
Baada ya hali hii chama cha TPTU kililazimika kuwatafuta waajiri wa shule za binafsi kupitia vyama vyao kama TAPIE,TAMONGSCO,CSSC,BAKWATA,BASUTA , hatua ambazo hazikuzaa matunda kwa kukosa ushirikiano kwa baadhi yao na wengine tuliofanikiwa kuwapata walieleza kuwa shule zao zimefilisika baada ya shule kufungwa kwa kuwa wanaziendesha kwa kutegemea ada za wanafunzi,hivyo hawana vyanzo vingine vya mapato vya kuweza kuwalipa walimu.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,baada ya hatua hizi kukwama tarehe 22/4/2020 tulilazimika kuiandikia barua Serikali yako barua yenye Kumb Na. RPRU/WOW/VOL 9/20 kupitia kwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, tukampa nakala Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof. Joyce Ndalichako,nakala nyingine pia tukampa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa Majaliwa tukiomba serikali ingilie kati kutatua tatizo hili, ili kunusuru hali mbaya ya maisha ya walimu na kila dhahama ya ukali wa maisha waliyokutana nayo ghafla baada ya kusitishiwa mishahara.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,baada ya barua kuiandikia serikali tulipokea simu ya msaidizi wa Waziri Mkuu aliyejitambulisha kwetu kwa jina la Bw.Mgalla akatueleza kuwa, wamepokea barua yetu na wameshamwelekeza cha kufanya Waziri wa Kazi, hivyo tuwe na subira kidogo suala letu linashughulikiwa.
Tulikaa kwa muda kusubiri mrejesho huo, tulipoona kimya tulianza kufanya ufuatiliaji kwa njia ya simu tukimpigia na kumtumia ujumbe wa maandishi Waziri wa Kazi ili kujua kipi kinaendelea, kwani hali ni mbaya kwa walimu, kutokana na ufuatiliaji huu tulipokea simu ya Kamishina wa Kazi nchini, Kanali Mbindi akituelekeza tusimsumbue Waziri kwa ujumbe mfupi na simu, kwani suala letu analo mezani, analishughukia tuwe na subira.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kadri siku zilivyokuwa zinaenda ndivyo hali ya maisha ya walimu ilizidi kuwa mbaya na tulikuwa bado hatujaambiwa chochote na serikali,hivyo tarehe Mei 13, 2020 tulilazimika kumwandikia barua Waziri Mkuu yenye Kumb Na. TPTU/WM/VOL.1/2020 tukimuomba afuatilie utekelezaji wa barua yetu tuliyomwandikia Waziri wa Kazi ili kuharakisha utatuzi wa mkwamo ambao unaathiri maisha ya walimu mtaani.
Hivyo kuwafanya wadharaulike na kuteseka,nakala za barua hii tulimpa Waziri wa Kazi,Waziri wa Elimu na nakala nyingine tulituma kwako.
Hali inayowafanya wavunjike moyo na kujihisi kuwa wanatengwa licha ya kazi yao kubwa na nzuri wanayofanya kwa Taifa hili,pamoja na hayo hata serikali bado haijajibu barua zetu tulizoandika kuomba msaada wa haraka wa kunusuru maisha ya walimu hawa ambao ni raia sawa na raia wengine wa nchi hii.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,haya ni mapendekezo yetu tuliyoiandikia Serikali ingilie kati kunusuru hali mbaya ya maisha ya walimu.
Mosi tulipendekeza Serikali iwaelekeze waajiri wa shule binafsi nchini,wawalipe walimu mishahara ya miezi Machi, Aprili na Mei na kisha Serikali ikutane na waajiri wa shule za binafsi na chama cha TPTU kujadili namna nzuri ya kuwasitiri hawa walimu na maisha yao kuanzia mwezi Juni kama Corona itaendelea kuwepo.
Pili waajiri wote wanaodaiwa malimbikizo ya nyuma ya mishahara kabla hata ya Corona haijaja tangu mwaka jana na kuendelea, tulishauri serikali iwaelekeze walipe malimbikizo hayo, kwani waliyalimbikiza kabla ya Corona kuja, hivyo wasitumie Corona kuwaumiza walimu.
Tatu waajiri wote waliokuwa wamesitisha mikataba ya walimu na kutoa barua za likizo bila malipo,hii ni kinyume kabisa ya sheria za kazi,tuliishauri serikali iwaelekeze kubatilisha hatua hizo na shule zikifunguliwa wawarudishe kazini walimu wote waliositishiwa mikataba.
Nne tuliishauri Serikali kukutana na waajiri wa shule binafsi na chama cha TPTU ili kujadili kwa pamoja namna nzuri ya kuwasaidia walimu hawa hasa kujikimu na maisha yao kuanzia mwezi Juni, mwaka huu kama Corona itaendelea kuwepo na sio kuwaacha hivyo.
Tano tuliishauri Serikali kupitia upya na kufumua mifumo ya ajira za sekta binafsi kutoka kuwa ni ajira za hisani za watu na kuwa ajira zinazozingatia vigezo na sheria za nchi,kwani lengo la Serikali kuruhusu watu kuwekeza ni kwa ajili ya kuzarisha ajira zenye vigezo zinazowanufaisha watanzania na sio kuwafanya watumwa.
Sita tuliishauri serikali kuwa mishahara yote ya wafanyakazi wa sekta binafsi hususani shule binafsi ilipwe kupitia taasisi za kifedha kama benki na sio ilivyo kwa sasa kwa baadhi ya waajiri hulipa walimu mishahara mkononi,hivyo serikali inakosa kodi za PAYE kwa shule nyingi na hata Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLP) inapoteza marejesho ya mikopo ya wanufaika waliopo kwenye ajira zenye taratibu hizi.
Jambo la saba,shida kubwa sana katika sekta binafsi hasa shule za binafsi waajiri wengi hawatoi mikataba kwa walimu hivyo kupelekea walimu hawa kupoteza haki zao nyingi za kikazi,hivyo tuliishauri Serikali kusimamia suala hili kuwa la lazima kila mwajiri anapoajiri lazima asainishe mfanyakazi wake mkataba wa kisheria ili kulinda haki na maslahi ya pande zote mbili na sio kama ilivyo kwa sasa mpaka hisani ya mtu au mwajiri mpaka ajisikie mwenyewe kutoa mikataba kwa wafanyakazi.
Tisa, ni wazi kabisa kuwa ‘minimum standard labour’ ambazo kimsingi zilipaswa kusimamia kwa kila mwaajiri na zingeepusha changamoto hizi hazijaweza kutekelezwa kwa sababu ya ongezeko la wafanyakazi na waajiri,hivyo tuliishauri serikali kuwa ianzishe idara maalumu inayosimamia ajira za sekta binafsi tu ili kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji,usimamizi na ukaguzi kwani maafisa kazi walioko mikoani wameelemewa na kundi kubwa la wafanyakazi na waajiri wa umma na sekta binafsi hivyo ufanisi wa usimamizi lazima upungue na kuruhusu mianya kama hii ya watu kuzikanyaga sheria watakavyo.
Jambo la 10,Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) inapoteza fedha nyingi kutoka sekta binafsi kutokana na wanufaika walioingia huku taarifa zao hufichwa fichwa ili kukwepa marejesho haya na hivyo kuwafanya wanufaika wengine wakose mikopo,tuliishauri Serikali kuwataka waajiri wote wa sekta binafsi hasa shule binafsi watoe ushirikiano wa dhati juu ya wanufaika hawa walionao ili mikopo hiyo irudi na wengine wakanufaike.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,haya ndiyo yalikuwa mapendekezo yetu tuliyoiandikia Serikali yako sikivu ambayo imekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi na haki za wanyonge kama sisi.
Tunaamini haya yakifanikishwa, itakuwa hatua za kutatua mkwamo uliopo na kutengeneza kesho nzuri juu ya ajira za shule binafsi hapa nchini,ni maombi yetu kwako kuwa mapendekezo yetu haya uyapokee na ikikupendeza uyatolee maelekezo ili hawa walimu na wao wafutwe machozi kama ulivyokuwa bega kwa bega na walimu wa shule za umma pamoja na watumishi wengine wa umma mpaka sasa Serikali yako imekuwa bega kwa bega nao.
Tunatanguliza shukrani za dhati.
Kwa niaba ya walimu shule binafsi nchini.
Julius Nkwabi Mabula
Katibu Mkuu
TPTU
More Stories
Tanzania Yaibuka Kidedea: Uongozi wa Rais Samia waboresha weledi wa Jeshi la Polisi
Tuhimize amani kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
Ana ahidi,ana tekeleza,maneno kidogo,vitendo vingi