November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barrick yaipa Serikali bilioni 250

Ni sehemu ya patano kuhusu fidia ya kodi, utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa Januari 24,2020

Na Joyce Kasiki, Dodoma

KAMPUNI ya Barrick imekabidhi kwa Serikali ya Tanzania hundi ya Dola za Kimarekani milioni 100 sawa na sh. bilioni 250 ikiwa ni sehemu ya malipo ya awali ya kiasi cha Dola milioni 300 sawa sh. bilioni 750 kama malipo ya Patano kuhusu fidia ya kodi.

Hundi ya kiasi hicho cha Dola za Marekani milioni 100 sawa na sh. bilioni 250 ilikabidhiwa jana jijini Dodoma kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

Tukio hilo ni mwanzo wa safari muhimu katika utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya serikali ya Tanzania na ya Barrick yaliyofikiwa Desemba 19, 2019 na kusainiwa rasmi Januari 24, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa masuala yaliyokubalika kwenye makubaliano hayo ni pamoja na Barrick kulipa dola milioni 300 za kimarekani kwa Serikali ya Tanzania kama malipo ya Patano kuhusu fidia ya kodi kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.

Pia pande husika zimekubaliana mpango wa malipo wa bakaa ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 200.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Mpango amesema; “Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania napenda kutoa shukrani za dhati kwa Kampuni ya Barrick kwa kuonesha dhamira ya dhati ya ushirikiano mzuri kwenye muelekeo mpya wa sekta ya madini Tanzania ambao umekubalika na pande zote kwa manufaa ya pande zote husika.

Mbali na makubaliano yaliyofikiwa, Kampuni ya Barrick ilikubali kufanya; kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 5 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Mtambo wa kuchakata madini nchini (Smelter) na kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutoa hadi dola za marekani milioni 10 kwa kipindi cha miaka kumi kwa ajili ya utoaji wa mafunzo yanayohusu sekta ya madini.

Mengine ni kutoa hadi dola za marekani milioni 6 kwa kila ounce ya madini itakayouzwa (ikijumuisha mchango kwenye Mfuko wa Maendeleo ulioanzishwa na Kampuni ya Barrick Tanzania) ili kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya migodi na kutoa kiasi cha dola za marekani milioni 40 kwa ajili ya kuboresha kipande cha barabara kati ya Bulyanhulu na Mwanza na kujenga nyumba na miundombinu yake.

Dkt. Mpango amesema wanaamini kwamba, pande zote mbili zinazohusika katika makubaliano zitaheshimu makubaliano na kuhakikisha yanatekelezwa.

“Nawahakikishia kwamba kwa upande wa Serikali ya Tanzania imedhamiria kwa dhati kutekeleza makubaliano hayo. Na kama ilivyoshuhudiwa hivi karibuni Serikali imeruhusu makontena na makinikia ya madini 277,” amesema Dkt. Mpango na kusisitiza;

“Tukio la leo ni hatua muhimu katika Sekta ya madini nchini ikizingatiwa kuwa Kampuni ya Barrick ni mdau muhimu katika Sekta hii. Nawaomba Kampuni nyingine za madini na wawekezaji wengine katika Sekta hii kufuata mfano mzuri uliooneshwa na Kampuni ya Barrick katika kuhakikisha kunakuwa na hali ya usawa (win- win Situation) katika uendeshaji wa shughuli za madini,” amesema Waziri Mpango.

Amesema Serikali ya Tanzania imedhamiria kwa dhati kuwa na ushirikiano wenye usawa katika Sekta ya madini utasaidia kuleta fedha ambazo zitasaidia katika kuboresha maisha ya Watanzania.