January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baraza la madiwani Halmashauri ya jiji la Tanga laridhia kusimamishwa kwa madiwani wawili

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online Tanga

Baraza la madiwani wa Halmashauri ya jiji la Tanga limeridhia kusimamishwa kwa madiwani wawili baada ya kuhusishwa na vitendo vya kumdharau naibu meya wa halmashauri ya jiji hilo Joseph Colvas kwenye kikao cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 kilichoongozwa na Naibu Meya wa jiji hilo Joseph Colvas.

Madiwani hao waliosimamishwa ni Habiba Namalecha diwani wa viti maalumu na Swalehe Mwagilo diwani wa kata ya Kirare.

Madiwani hao wamesimamishwa hadi mwezi April 2023 ambapo hawatohudhuria katika vikao vitatu vya mabaraza pamoja na kukosa stahiki zao.

Akitoa taarifa hiyo katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2021/2022 kilichofanyika jijini Tanga Mstahiki Meya wa halmashauri ya Jiji la Tanga Abdulrahman Shiloo mara baada ya Baraza kugeuka kamati kwajili ya kujadili maswala ya kinidhamu.

Meya Shiloo amesema wamechukua hatua hiyo ili madiwani hao kuwa mfano kwa madiwani wengine ambao wanakosa nidhamu kwa viongozi wao.

Aidha Meya Shiloo alisema kuwa madiwani hao hawatahudhuria vikao vitatu vya kanuni pamoja na kukosa stahiki zao ambapo watatakiwa kurejea kwenye baraza hilo kwenye kikao cha mwezi wa nne 2023.

“Wajumbe 22 kati ya 28 waliohudhuria kikao hicho walimshauri Mstahiki Meya kuchukua adhabu dhidi ya madiwani hao ili iwe fundisho kwa madiwani tunaobaki na kulifanya Baraza letu liwe lenye nidhamu na kuleta maslahi kwa wananchi” alisema Shiloo.

Shiloo alisema kuwa kutokana na kanuni za baraza hilo madiwani hao hawatahudhuria vikao vitatu vya mwezi wa saba, wa kumi na wa kwanza pamoja na vikao vingine vinavyohusiana na kamati vya kuandaa mabaraza hayo.

Hata hivyo mstahiki Meya Shillow aliwataka madiwani hao kuheshimu mamlaka na sheria zilizopo katika kuongoza baraza hilo pamoja na sehemu nyingine ili kuweza kutatua changamoto zilizopo kuwa maslahi mapana ya wananchi.

“Nataka mamlaka yangu mliyonikabidhi nyinyi nyinyi wenyewe na ya naibu wangu myaheshimu wote na muyatii na Mamlaka ya yeyote yule atakayepewa dhamana ya kuliendesha baraza hili, haina maana Meya asipokuwepo baraza lisiendeshwe hilo halikubaliki” alisema Meya Shiloo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja mstaafu Hamis Mkoba amewataka madiwani na watumishi wa halmashauri kuheshimu mamlaka ili kuepukana na migogoro inayoweza kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.

“Madiwani mnatakiwa kwanza mnatakiwa muwe kitu kimoja na hamuwezi kuwa kitu kimoja kama hamuheshimiani, “alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amewataka madiwani kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo baada ya kubainika kuwa halmashauri hiyo imepatiwa miradi mingi ya maendeleo.

Katika haua nyingine Mgandilwa amewataka madiwani hao kuhamasisha wananchi suala la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni kwa kile alichodai kukamilika kwa zoezi hilo ndio msingi wa maendeleo wa Taifa.