December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bandari ya Tanga yaanza kuhudumia meli kubwa ya mizigo

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Bandari ya Tanga imeanza kuhudumia meli kubwa ya mizigo yenye urefu wa mita 179 meli ambayo imekuja na magari ikiwa ni mara ya kwanza kushushwa magari bandarini hapo baada ya maboresho ya ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 450.

Meli hiyo iliyotokea Nchini China ni meli ya kwanza kuja na magari katika bandari ya Tanga tofauti na meli nyingine ambazo zilishakwisha kutia nanga bandarini hapo mara baada ya kukamilika kwa maboresho hayo.

Ukiachana na meli kubwa yenye urefu wa mita 150 iliyopokelewa hivi karibuni katika bandari ya Tanga imeendelea kuwa mwendelezo ambapo bandari hiyo kwa mara nyingine imepokea meli yenye urefu wa mita 179 kutoka Nchini China iliyobeba magari na vifaa vya kiwanda cha Maweni Lime stone kilichopo Mkoani hapa huku wakitarajia kupokea meli nyingine yenye urefu wa mita 189.9 hii ikionyesha mapinduzi ya kibiashara ambayo yatazidi kuifungua Tanga.

Mkuu mpya wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amewataka wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuitumia bandari ya Tanga hasa mara baada ya ukamilishaji wa ujenzi wa gati la kisasa lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za mizigo tofauti na hapo awali.

Waziri Kindamba ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara yake katika bandari ya Tanga ikiwa ni ziara ya kwanza anayoifanya mara baada ya kuhamishiwa kwenye Mkoa huo ambaye amekuja na kauli mbiu ya ‘Tanga lango kuu la Afrika Mashariki’.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa wanaitazama bandari ya Tanga kimkakati zaidi na kuwaasa wafanyabiashara mbalimbali wa kutoka ndani ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki kuitumia bandari ya Tanga ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwao katika kusafirisha mizigo yao kwa haraka zaidi.

“Niwaombe wafanyabiashara wote wa ndani na nje ya Tanga kutumia bandari yetu ya Tanga lakini pia niwasisitize majirani zetu wa Rwanda, Burundi, Congo, Kenya na kwingineko waangalie bandari ya Tanga kama changuo lao namba moja, “alibainisha Kindamba.

“Bandari hii ndio moyo wa uchumi wa Mkoa wa Tanga sisi kama wasimamizi wa serikali tunakwenda kuisimamia bandari hii kwa ukaribu zaidi tunataka Dunia ijue kwamba ipo bandari inayoitwa bandari ya Tanga tena ikiwa na usalama mkubwa kabisa, “alisisitiza Kindamba.

Kwa upande wake Meneja wa bandari ya Tanga Masoud Mrisha amemuomba Mkuu wa Mkoa kusimamia upanuzi wa miundombinu ya barabara ndani ya jiji la Tanga kwa lengo la kuepusha msongamano wa magari wakati biashara itakaposhamiri bandarini hapo.

“Niiombe Serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini Tarura na Tanroads kutengenezwa kwa miundombinu ya barabara ya kilomita 7 inayokwenda Mwambani kwenye bandari ndogo kule tunatarajia kujenga sehemu ya kuhifadhia mizigo yetu sote tunafahamu bandari yetu ya Tanga ina ukubwa wa hekta 17 eneo hili sio kubwa sana tumemwomba mkuu wa mkoa atusaidie kututilia nguvu kwenye hizo taasisi” alisema Mrisha

Aliongeza kuwa niwaombe wafanyabiashara na wateja wanaotumia bandari ya Tanga sasa waje kuitumia bandari yetu ya Tanga kwani serikali imefanya maboresho makubwa katika bandari hii ambapo hivi sasa imeanza kupokea meli kubwa, “alisema Mrisha.

Serikali imewekeza kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 429 kwenye bandari ya Tanga kwajili ya ujenzi wa gati, kuongeza kina cha maji na ununuzi wa mitambo kwajili ya kuwezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa ambazo zilikuwa zinashindwa kutia nanga bandarini hapo.

Hata hivyo serikali inatarajia kufanya uzinduzi rasmi wa mradi wa gati katika bandaro hiyo ifikapo mwezi April mwaka huu.