Na Mwandishi Wetu,Busan, Korea Kusini
BALIZI na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UNESCO, Saidi Yakubu, amekutana na mwakilishi wa Tanzania katika Jukwaa la Vijana Wataalamu wa Urithi wa Dunia 2026, Rose Kinabo, pembezoni mwa Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea jijini Busan, Korea Kusini.
Katika mazungumzo yao,Balozi amempongeza Kinabo kwa kuiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa hilo la kimataifa, baada ya kuchaguliwa miongoni mwa washiriki wachache kutoka mataifa 29 waliopatikana kupitia mchakato wa ushindani mkubwa wa kimataifa.
Kinabo, ambaye ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mtaalamu wa usimamizi wa urithi kwa kushirikisha jamii, aliwasilisha uzoefu wa Tanzania kuhusu usimamizi shirikishi wa maeneo ya urithi na mchango wa taasisi za elimu katika kulinda na kuendeleza urithi wa dunia. Uwasilishaji wake uliendana na kaulimbiu ya jukwaa la mwaka huu: “World Heritage, Communities and Education: Empowering Youth as Agents of Change.”
Balozi Yakubu ameeleza kuwa ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo umeendelea kuonesha uwezo wa wataalamu na vijana wa Kitanzania katika kuchangia mijadala ya kimataifa kuhusu uhifadhi wa urithi wa dunia, huku ukiimarisha nafasi ya Tanzania ndani ya UNESCO.

Katika kikao hicho,Balozi aliambatana na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Profesa Hamisi Malebo, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania unaoshiriki Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia.
Ushiriki wa Rose Kinabo umechangia katika maandalizi ya Azimio la Vijana la UNESCO kuhusu Urithi wa Dunia, litakalowasilishwa rasmi mbele ya Kamati ya Urithi wa Dunia, na kuendelea kuitangaza Tanzania kama mdau muhimu katika kulinda na kuendeleza urithi wa dunia kupitia elimu, ushirikishwaji wa jamii na uongozi wa vijana.

More Stories
HGWT yaahidi kutekeleza mkakati wa kutokomeza ukeketaji
Alizeti yawa zao kimbilio kwa wakulima Chunya
Askari wanyamapori Babati wapata mafunzo