December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi: Sekta ya habari nguzo muhimu ukuaji demokrasia

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Wiebe de Boer amesema kuna juhudi kubwa ambazo zimefanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambazo zimeimarisha uhuru wa vyombo vya habari.

Balozi Boer ameyasema hayo jana Oktoba 20, 2022 jijini Dar es salaam wakati akifungua mafunzo maalumu ya siku moja kwa wahariri na wanahabari yanayoangazia uchechemuzi wa sheria za vyombo vya habari nchini ambayo yanaratibiwa na jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) .

Balozi Boer amesema uhuru wa vyombo vya habari nchini ni nguzo mojawapo muhimu katika kuchochea ukuaji wa maendeleo kiuchumi na ustawi bora wa demokrasia.

“Vyombo vya habari vinafanya kazi ya kujenga uelewa katika jamii , kuwafanya wananchi kufanya uamuzi kutokana na uelewa walionao hivyo wanapokuwa na uelewa mkubwa katika jamii na mambo mbalimbali demokrasia itakua kwasababu watafanya uamuzi wakijua kwamba wanamtaka fulani si kwasababu amewapa kanga au kifua wakati wa kampeni, lakini ameahidi kujenga miundombinu, kukuza mfumo wa elimu na uchumi jambo ambalo litasaidia siyo tu mtu mmoja mmoja bali kizazi na taifa kwa ujumla” amesema.

Aidha Balozi Boer amewataka wanahabari nchini kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhamasisha mazingira wezeshi ya upatikanaji wa habari nchini.

Pia Balozi Boer aliwapongeza TEF kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa na elimu juu ya umuhimu wa maboresho ya sheria za habari nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Deodatus Balile ameishukuru serikali kwa kuonyesha utayari wa kufanya maboresho ya sheria ya habari nchini.

“Lazima tuwe na moyo wa shukrani kwa serikali, tumeona magazeti mbalimbali yakifunguliwa na kuna juhudi mbalimbali zinaendelea ili kuhakikisha kwamba sheria ambazo zinaonekana kubinya uhuru wa vyombo vya habari zinafanyiwa maboresho”

Ikumbukwe kuwa Mei 3, mwaka huu, wakati Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alihutubia katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari ikiongozwa na Kaulimbiu isemayo ‘ Uandishi wa habari na Changamoto za kidigiti’ alielekeza sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote.