Na Penina Malundo,Timesmajira
KATIBU Mkuu Kiongozi Mstaafu wa Tanzania,Balozi Ombeni Sefue amesema ili nchi za Afrika zifanikishe kutoa elimu bora ni vema kuwekeza kwenye elimu zaidi hususan katika bajeti zao kwani Afrika imekuwa ikiwekeza kiwango kidogo kwenye masuala ya elimu ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea.
Pia amesema nchi hizo za afrika zinatakiwa kuzingatia uwekezaji endelevu na imara zaidi kwenye elimu,ukumbatiaji wa teknolojia na masuala ya akili mnemba(AI)pamoja na mabadiliko ya sera za elimu.
Balozi Sefue ameyasema hayo jana mjini Kampala,Uganda wakati akiwasilisha mada kuhusiana na maendeleo endelevu ya kiafrika katika upande wa elimu katika kongamano la 8 la Uongozi wa Afrika (ALF)lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi amesema nchi nyingi za kiafrika zimeweka bure utoaji wa elimu kwenye eneo la ada tu,huku gharama nyingine zimekuwa zikitolewa na mzazi hali ambayo kaya maskini kushindwa kumudu kuwapeleka watoto wao shuleni.
”Kuna vizuizi vingi vya kujiunga na elimu kwa nchi za Afrika,ikiwemo uhaba wa shule za msingi,Changamoto za masuala ya kitamaduni na kijamii kama vile ndoa za mapema,mimba za utotoni,upendeleo wa kielimu kwa wavulana pamoja na Changamoto za miundombinu shuleni.
”Ni ukweli nchi nyingi za kiafrika zimewekeza bure utoaji wa elimu ila katika gharama nyingine kama vile sare,Madaftari na vingine, mzazi mwenyewe anatakiwa kuwajibika hali inayosababisha kaya maskini kushindwa kumudu hayo na kushindwa kuwapeleka watoto shuleni,”amesema.

Balozi Sefue amesema inapozungumziwa suala la elimu bora ni kuondosha mfumo wa zamani wa kielimu na mitaala yake hususan elimu ya juu na kuwa na elimu ya kuzalisha kazi badala ya kuwa watafutaji wa kazi.
”Ili kufanikisha haya Afrika inaweza kutoa mafunzo zaidi kwa walimu kwani walimu wengi wa nchi za kiafrika wamekua na uwezo mdogo kwenye utoaji wa elimu ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea.
”Pia uwepo wa shule jumuishi na zinazofikika kwa urahisi,shule ambazo zitawezesha hata watu wenye ulemavu kupata elimu kwa urahisi kwa kufanya hivyo itasaidia kuongezaa ubora wa elimu,”amesema Balozi Sefue.

Aidha amesema pia nchi za afrika zinaweza kutoka zilipo sasa na kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kidijitali hivyo kuinua viwango vya elimu kwa afrika kwa kiasi kikubwa.
Awali akifunga jukwaa hilo,Waziri Mkuu wa Uganda,Robinah Nabbanja amesisitiza wajumbe wa jukwaa hilo kuwa kila kilichojadiliwa katika jukwaa hilo kikafanyike kwa vitendo na sio kuishia hewani kwaajili ya maendeleo endelevu ya afrika.
Amesema ili kufikia hayo yote ni vizuri suala la ulinzi na amani kuendelea kudumisha katika nchi ao kwani hauwezi kufikilia maendeleo kama nchi yako haina amani.

Akizungumzia suala la kilimo,Nabbanja amesisitiza uwekezaji zaidi katika kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha zaidi na kuuza bidhaa nje ya bara la Afrika na kuendelea kukuza uchumi wa nchi zao .
”Tunatakiwa kuendelea kuunganisha Afrika yetu kwa barabara,reli pamoja na Usafiri wa majini ili kufanya biashara huru baina ya Nchi hizi na kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji ambapo kwa namna moja au nyingine watazalisha ajira kwa wingi kwa vijana wetu.
”Pia tunapaswa kutengeneza mazingira rafiki kwenye uzalishaji wa umeme ili gharama za umeme zishuke na zikishuka zitasaidia ukuaji wa maendeleo endelevu na kuendelea kuvutia wawekezaji na kukuza ajira zetu,”amesema
More Stories
Doreen: ‘Msiwafiche watoto wenye utindio wa Ubongo
Serikali yawezesha miradi 80 kwa utaratibu wa PPP
Mpogolo akabidhi Cheti kwa wahitimu