November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Nchimbi aonya viongozi kutoa kauli za kibaguzi

Na Mwandishi Wetu. Iringa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewataka viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuepuka kutoa kauli au kufanya vitendo vyenye taswira inayoweza kutafsiriwa kuwa baadhi yao wanashabikia ukandamizaji wa haki za wananchi.

Katibu Mkuu huyo, Balozi Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa maneno na vitendo vya wana-CCM wakati wote lazima yaakisi dhamana ambayo chama kimepewa na wananchi ya kuwatumikia, ikiwemo kusimamia haki, bila ubaguzi wala dhuluma ya aina yoyote .

Balozi Nchimbi amesema hayo akiwa Chuo cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) leo, Julai 11, 2024 Ihemi, mkoani Iringa, alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa jumuiya hiyo wa ngazi za mikoa na wilaya zote, nchi nzima, leo Alhamis, 11 Julai 2024.

“Suala jingine ninataka kuwasisitiza UVCCM ni umuhimu wa watendaji wetu, viongozi wetu na wanachama wetu kutambua kuwa mnabeba taswira ya Chama chetu kila wakati, katika mnayosema au kutenda. Kama kuna jambo tunapaswa kulilinda kwa wivu mkubwa ni taswira chanya ya CCM, hasa jambo linalohusu dhamana ya kuongoza nchi yetu na kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa, kwa kupinga kauli na vitendo vya ubaguzi na dhuluma kwa Watanzania,” amesema Balozi Nchimbi.

“Ninyi UVCCM mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda taswira hiyo muda wote. Tujiepushe kabisa na kauli au matendo yanayoharibu taswira ya CCM. Katika kila unachokisema au kukitenda lazima utafakari, je kina athari gani kwa CCM na nchi yetu.” ameongeza

Aidha, katika kulinda dhima hiyo ya CCM, Balozi Nchimbi amewakumbusha wana-CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa, hadi sasa hakuna chama kingine tofauti na CCM kimeonesha uwezo wa kuongoza nchi na pia wananchi hawako tayari kufanya majaribio kwa vyama vingine ambavyo havina mwelekeo, hali ambayo ni hatari kwa uimara wa nchi

Vilevile, Balozi amewapongeza UVCCM kwa kuweka ‘rekodi’ mpya ya kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa walipozindua mkakati wao wa “Tunazima Zote, Tunawasha Kijani”, akiwataka wasonge mbele, watumie ushawishi walionao kwa vijana nchini, kwa uaminifu na uadilifu huku wakitambua kuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa na vijana.

Awali akimkaribisha Balozi Nchimbi, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Komredi Mohammed Ali Mohammed (Kawaida), amekishukuru Chama chini ya Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi kinavyoendelea kuwalea na kuwaamini vijana kukitumikia Chama na jumuiya zake na nchi kwa ujumla.

Nae Katibu Mkuu wa UVCCM, Komredi Joketi Urban Mwegelo akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya mafunzo hayo, amesema yatawasaidia viongozi na watendaji wa jumuiya hiyo kwenye mikoa, wilaya na hatimae kushuka ngazi zingine nchi nzima kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi unaohitajika.