March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Dkt Kusiluka awahimiza maafisa Habari kuzingatia weledi, uzalendo

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, amewataka Maafisa Habari wa Serikali nchini kuzingatia weledi, maadili na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, pamoja na kulinda maslahi ya Taifa katika kipindi chenye kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Akizungumza leo Desemba 17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao Kazi cha Kitaifa cha Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Maafisa Habari wa Serikali, chenye kauli mbiu “Utu na Mawasiliano yenye Uwajibikaji”,
Balozi Dkt. Kusiluka amesema Serikali inawategemea Maafisa Habari kama jeshi muhimu katika kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa ufasaha.

Amesema jukumu hilo ni muhimu hasa katika mazingira ambayo taarifa potofu na propaganda zinaweza kuhatarisha usalama, amani na mshikamano wa nchi endapo hazitadhibitiwa ipasavyo.

” Maafisa Habari mnapaswa kutoa taarifa sahihi kuhusu kazi, mipango na mafanikio ya Serikali, sambamba na kukusanya kero za wananchi na kuzifikisha kwa wahusika ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati”amesema Balozi Dkt Kusiluka

Ameeleza kuwa kikao hicho kimeandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha viongozi wapya na wataalamu wa habari mapema, kujenga uelewano wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuweka msingi imara wa ushirikiano katika kusukuma mbele ajenda ya Serikali.

Aidha, amesema maendeleo ya teknolojia ya habari yameleta fursa kubwa lakini pia changamoto, akionya kuwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yanaweza kuleta madhara endapo hayatatumika kwa weledi na uzalendo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bakari Machumu, amesema katika mazingira ya sasa yenye changamoto na kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa Serikali kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za msingi kuhusu mafanikio na mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema kufanya hivyo husaidia kuelekeza mjadala wa umma, kupunguza upotoshaji wa taarifa na kuongeza uelewa pamoja na imani ya wananchi kwa Serikali.

Naye Mshauri wa Rais masuala ya habari, Tido Muhando, amesema mawasiliano yanayozingatia ukweli, uwiano na uwakilishi wa maeneo yote ya nchi ni nyenzo muhimu katika kumsaidia Rais na Serikali kuelewa hali halisi ya wananchi na kuimarisha ufanisi wa mawasiliano ya Serikali kwa ujumla.