Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Imeelezwa kuwa Waandishi wa habari ni watu muhimu katika kutetea na kusimamia Demokrasia nchini hivyo wameshauriwa kuandika habari zinazotetea taaluma yao na maslahi yao kwa ujumla.
Hayo ameyasema Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile wakati wa semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na jukwaa hilo kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu utetezi wa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari nchini.
“Waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kutetea taaluma yao na maslahi yao kwa ujumla lakini zipo baadhi ya sheria zinasababisha kushidwa kufanya kazi zao kwa weledi na hivyo kushidwa kutetea haki na maslahi yao.”
Kuhusu vifungu vya sheria ya habari, Balile amesema kuwa wapo kwenye mchakato wa kuona namna ambavyo Bunge litapitia upya sheria hizo hususani ni zile zinazoleta vikwazo kwa waandishi wa habari ili vifanyiwe marekebisho.
Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF, Theophil Makunga amesema Waandishi wa habari ni watu muhimu katika kutetea na kusimamia Demokrasia katika nchi endapo watafanya kazi yao kwa uhuru na demokrasia inakua huru zaidi .
Makunga aliishukuru serikali kwa kuonyesha mwanga wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo ya habari nchini.
“Tunashukuru kwamba serikali imeliona hilo na imekubali kuongea na vyombo vya habari kurekebisha baadhi ya vipengele ambavyo tunafikiri vinawabana waandishi wa habari”
“Naamini kwamba tunapoelekea kuna mwanga unaonekana mbele wa kuwafanya waandishi wa habari waweze kufanya kazi kwa uhuru ili kuleta maendeleo ya nchi “
Makunga amesema Mwandishi wa habari mahali popote ni muhusika katika maendeleo na siyo kwamba ni mdau katika maendeleo au mpinzani katika maendeleo hivyo unapompa nafasi ya kufanya kazi yake kwa uhuru inamaana inamsaidia kusukuma maendeleo katika nchi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best