Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema, mabadiliko ya sheria za habari nchini, bado yanahitajika kwa kiasi kikubwa.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipohojiwa kuhusu hatua zilizofikiwa mpaka sasa katika safari ya mabadiliko ya sheria hizo.
Amesema, kasi ya sasa ya kuendea mabadiliko hayo imesinyaa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Amemwomba Nape Nnauye ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliasiliano na Teknolojia ya Habari kuongeza kasi ili kufikia malengo.
Balile amesema, kasi iliyopo sasa inatia mashaka kukamilika kwa mchakato huo kabla ya Bunge la Mwezi wa Tisa.
“Hapo awali tulikwenda vizuri, lakini tangu baada ya Mei 3 mwaka huu (Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani), tunaona kasi imepungua kidogo,” amesema Balile.
Amesema, awali serikali kupitia Wizara ya Habari chini ya Nape, ilipanga kufanya vikao mbalimbali na wadau wa habari, lakini mpaka sasa havijafanyika.
“Bado tunazihitaji sheria, bado tunahitaji hayo mabadiliko haraka kadri inavyowezekana kuliko wakati wowote ule kwa sababu, tukipitwa na lile bunge la mwezi wa tisa, ina maana tutasubiri mwaka mmoja baadaye. Bunge la mwezi wa tisa ndio la miswada,” amesema.
Pamoja na kuchelewa huko, Balile amasema iwapo wizara uenye dhamana ikiamua sasa kuongeza kasi katika mchakato huo, upo uwezekano mkubwa wa kufikia malengo ndani ya muda muafaka.
“Tunachotafuta zaidi ni haki ya kupata habari na uhuru wa vyombo vya Habari. Huu uhuru unawezesha haki nyingine kupatikana. Mfano demokrasia na vingine vyote vinavyozungumzwa, vinatokana na uhuru wa watu kutoa mawazo yao.
“Inapokuwa uhuru haujalindwa kisheria, basi unachelewesha hivi vingine kupatikana katika jamii. Huu ni mjadala na mchakato tunaopaswa kushirikishana tulio wengi kwa Pamoja,” amesema.
Hata hivyo, Nape akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo kusaidia ukuaji wa habaro tarehe 13 Julai 2022 alisema, serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuwasilisha mbadala wa maoni yao na kwamba, na ina malengo ya kuukamilisha mchakato huo kwa muda mfupi.
“Serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuleta mbadala wa yale yanayolalamikiwa, tukae mezani tuzungumze na huo mchakato haiwezi kuwa mfupi, ni chakato wa mazungumzo, mie nimeukuta na tuaendelea nao. Tuna malengo ya kuukamilisha mapema kadri inavyowezekana,” alisema Nape na kuongeza;
“Sheri ya habari ilipotungwa, ililenga kutatua matatizo ya habari ikiwemo ajira zao, maslahi yao, mazingira yao ya kazi, haki zao na wajibu wao. Sasa inawezekana masuluhisho yaliyopo kwenye sheria, ndio yanayogombaniwa kwamba ni sahihi ama si sahihi.”
Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali alisema, serikali imeonesha dhamira ya kutaka kupitia upya sheria na taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari 2016.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini