December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bakwata,Jiji la Mwanza wakutana kuzungumzia kiwanja cha madarasa Muslim

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) na Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wako kwenye mazungumzo ya kiwanja cha Madrasa Muslim kinachomilikiwa na taasisi hiyo. 

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke amesema  leo jijini humo wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusiana na mazungumzo yanayoendelea kati ya taasisi hiyo na Jiji.

“Kwanza tulifanya dua ya kumshukuru Mwenyezi Mungu baada ya kushinda kesi ya umiliki wa kiwanja cha Madrasa Muslim  iliyodumu kwa miaka kadhaa,pia kuishukuru na kuipongeza mahakama kuendelea kuwa mhimili bora wa kutoa haki na Kuiwezesha BAKWATA  kupata haki yake dhidi ya  Halmashauri ya Jiji la Mwanza,”amesema.Sheikhe Kabeke.

Amesema walishinda kesi ya kiwanja kilichokuwa kikibishaniwa kati yao na Jiji, Mahakama ikatoa uamuzi kuwa ni mali ya BAKWATA ambapo  mwaka 2022 walikaza hukumu.

Baada ya kukaza hukumu mahakama ilitoa masharti mawili ndani ya siku 90  moja ni endapo Jiji inakihitaji iwalipe fidia ya milioni 539 na pili wakishindwa wakiachie na kukirejesha BAKWATA lakini ndani ya siku hizo yote hayakutekelezwa.

Pia baada ya muda huo kupita BAKWATA kupitia Wakili wake, Hamisi Magongo aliiandikia Halmashauri ya Jiji barua mara kadhaa kuwakumbusha lakini hazikujibiwa.

“Kwa ukimya huo na ili kulinda uhusiano  wa BAKWATA na Jiji nilijitahidi binafsi kukutana na viongozi wao bado hakukuwa na jibu lolote, hivyo Waislamu walielezwa wakatoa mwongozo wa nini kifanyike kwenye kiwanja hicho na endapo Jiji wanakihitaji walipe kwa bei ya soko licha ya kuwa kinatumika kwa huduma za jamii,”amesema Sheikhe Kabeke.

Amesistiza kwa mazingira hayo ambayo kwa miaka zaidi ya 15 wametoa sadaka katika eneo hilo la wakfu lililotolewa litumike kufundisha elimu ya dini kwa Waislamu ambapo wengi wao walisoma katika Madrasa iliyokuwa eneo hilo na baada ya  mazungumzo majibu yatatolewa ya nini wameafikiana.

“Tumekuwa na mazungumzo yanaendelea na watu wa Jiji na wengine wanaohitaji eneo hilo,BAKWATA ina viongozi makini na busara imetuongoza na tunawaomba waislamu wawe na subira wakati wa mazungumzo kisha tutarejea kwa waumini  kuwaeleza kilichojiri kwenye kiwanja hicho,”amesema Sheikhe Kabeke.