December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) Mkoa wa Singida, Burhan Mlau. akiwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Singida, Salum Mahami (kulia), akiongoza kuomba dua katika Swala ya Eid Al-Haji, Singida mwaka 2019. Picha ya Maktaba

BAKWATA yahimiza dua Mungu aepushe Corona

Na Jumbe Ismailly, Singida

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida limewaomba Waislamu mkoani Singida kutumia Quran tukufu kusoma dua ili Mungu aweze kuwaondolea Watanzania na duniani kwa ujumla ugonjwa wa Virusi vya Corona.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa BAKWATA wa Mkoa wa Singida, Alhaji Buruhani Mlau kwenye hafla ya kupokea vitabu vya Quran Tukufu vikiwemo misahafu 100 na juzuu 400 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi kwa tiketi ya CCM, Elibariki Kingu kwa ajili ya kugawa kwenye misikiti yote ya jimbo hilo.

“Quran hii ni kwa ajili ya kufanya dua ya kujikinga na ugonjwa wa Corona, kwani hakuna binadamu mwenye kuyaondoa maradhi haya ila ni Mwenyezi Mungu kupitia Quran hii tukufu,” alisisitiza Alhaji Mlau.

Aidha Katibu huyo wa BAKWATA alifafanua kwamba Juzuu hizo alizopokea watoto watazisoma, watamjua Mungu na Mtume Mohammad (SAW).

“Umenikabidhi leo hii (jana) ambayo ni siku ya pili ya funga yetu leo (jana), hivyo nitawapa Waislamu wote wa jimbo lako la Singida Magharibi na watasoma na kuomba dua katika misahafu hii,” alisema Katibu Mlau.

Hivyo Alhaji Mlau alitumia fursa hiyo kumuomba Mungu amjaalie Mbunge Kingu na kutoa wito kwa viongozi au wabunge wengine waige mfano wake wa kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu

Akikabidhi msaada huo, Kingu alisisitiza kuwa kipindi hiki ni cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hivyo katibu wa BAKWATA ndiye atakayesimamia ugawaji kwenye misikiti yote ya jimbo hilo ili waislamu waweze kusoma na kuomba dua ili janga Corona liweze kutoweka.

“Kwa niaba yangu,familia yangu,familia ya rafiki yangu Kuwingwa wa Manyoni pamoja na rafiki zetu waliopo Saudi Arabia tuliwaomba watupatie msaada wa juzuu pamoja na Corani takatifu kwa ajili ya kuwasaidia Waislamu tunapoelekea mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani waweze kuvitumia vitabu hivi kwenye misikiti yangu yote ya jimbo zima la Singida Magharibi,”alisema Kingu

Kwa mujibu wa Kingu endapo waumini hao wa dini ya kiislamu watatumia vitabu hivyo vitakatifu kuamudu Mungu pamoja na kuiombea Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli ili kuendeleza mshikamano wa Mkoa wa Singida.