Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,limekusanya zaidi ya sh.milioni 40.4, katika kilele cha siku ya Badri,zikiwemo ahadi na fedha taslimu za ujenzi wa vituo saba za afya,lengo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za jamii.
Machi 18,2025 Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke,katika kilele cha siku hiyo ya Badri, amesema ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa vituo vya afya zinahitajika kiasi cha bilioni 4.5.

Huku kiasi cha milioni 100 zimetolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, milioni 200 kutoka fedha za ndani na milioni 8.9 kutoka kwa wadau.
“Hapa zinatafutwa sh.bilioni 1.5 tuendeleze mradi huu,hivyo tusitishwe iwe mvua au jua hatushindwi lazima vituo vijengwe ili hata tukiondoka tuache alama,”amesema.
Sheikh Kabeke ameiomba Serikali za Wilaya ya Magu na Misungwi,ili kupata viwanja vya kujenga vituo vya afya huku akieleza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe tayari amewapatia kiwanja cha kujenga kituo.
Mgeni rasmi katika awamu ya pili ya ujenzi wa vituo saba vya afya, Sheikh wa Mkoa wa Simiyu, Issa Kwezi, amempongeza Sheikh Kabeke, kwa ubinifu huo, hivyo amewaomba wananchi wa Mkoa wa Mwanza kumuunga mkono ili kutekeleza mradi huo.
“Simiyu tumeiga na kujifunza kutoka Mwanza,huko nyuma hatukuwahi kuona gari la BAKWATA mtaani,sasa ujenzi wa vituo vya afya vinajengwa kwa ubunifu na weledi unastahili pongezi,”amesema Sheikh Kwezina kuongeza:
“Wasukuma kuna kitu wanaita ndhulu (choroko) hata ukizipika utakuta nyingine haijaiva,wapo watu hata uwapike vipi hawaivi, ukifanya mazuri hawayaoni wanaweza kukukwamisha,wakati mwingine unawasamehe tu,sisi Simiyu tutakuunga mkono kwa milioni 1,”.

Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini,Haruna Kambilo amechangia saruji mifuko 10,ambapo amesema anayoyafanya Sheikh Kabeke ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na anamuunga mkono Rais Samia katika maendeleo.
Diwani wa Kitongoni Kigoma Mjini,Himid Mkunda amechangia kiasi cha milioni 1,huku akiwataka waislamu kuwa na umoja.
Diwani wa Kisesa na Mwenyekiti Halmashauri ya Magu,Joseph Kabadi,kwa niaba ya Leonard Qwihaya (MNEC) amesema,jambo lililo fanywa na BAKWATA la kujenga vituo vya afya ni jambo la kijamii,ambapo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amechangia saruji mifuko 100,tripu 35 za mchanga na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono.

More Stories
Mo Dewji na Urithi anaoujenga ,unavyoenda mbali zaidi ya mafanikio binafsi
Mulika Community kusaidia Serikali kukomesha vitendo vya ukatili
TMDA yashinda tuzo za PRST ya Umahiri katika kampeni bora ya utoaji elimu jamii