May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BAKITA yapiga marufuku ufunguaji holela wa vituo vya kufundishia lugha ya kiswahili

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Baraza la Kiswahili la Taifa( BAKITA) limepiga marufuku ufunguaji holela wa vituo vya kufundisha lugha ya Kiswahili kwa raia wa kigeni bila ya kuwa na kibali cha BARAZA na kwa watakaokiuka utaratibu huo hatua kali zitakchukuliwa dhidi yao ikiwemo kufungwa kwa vituo vyao pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Ameyasema hayo leo Kaimu Katibu Mtendaji kutoka BAKITA Consolata Mushi wakati akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akitoa taarifa ya maadhimisho ya siku ya kiswahili Duniani yanayotarajiwa kufanyika siku ya tarehe 7/7/ 2022.

alisema lugha ya kiswahili ni lugha ya kwanza ya kiafrika kutambuliwa Umoja wa Mataifa na hivyo kutangaziwa siku yake maalumu ya maadhimisho ambayo itakuwa tarehe 07/07 kila mwaka;

“Kupitia vyombo vya habari, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Novemba 23,2021 lilitangaza kuwa lugha ya kiswahili imetambuliwa kama lugha rasmi miongoni mwake zikiwamo Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kirusi, Kispanyola na Kiarabu”

Aidha alisema hadhi ya kiswahili Duniani ni kubwa na hii ndiyo iliyosababisha kutengewa siku yake maalumu ambapo kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi Duniani na kwa sasa kina wazungumzaji zaidi ya Milioni 200 Duniani, kinafundishwa katika vyuo vikuu zaidi ya 58, Nchini Tanzania unaweza kusoma Shahada ya kwanza hadi ya uzamivu kwa kiswahili

Pia Consolata alizitaja sababu ya tarehe 7/7 ya kila mwaka kuwa muhimu kwa watanzania ambazo ni pamoja na Tarehe 7/7 Muasisi wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alianza kutumia kiswahili kama lugha kuwaunganisha watanzania katika harakati za kudai uhuru.

Aliongeza kuwa Tarehe 7 mwaka 2000 Jumuhiya ya Afrika Mashariki ilianza upya baada ya kuwa ulivunjika mwaka 1977 na tatu, 7/7 ni sabasaba ambayo ni maonesho ya biashara kimataifa nchini kwahiyo kiswahili ni zana ya biashara

Aidha Consolata alisema Serikali kupitia BAKITA imepanga mambo yatakayofanywa katika siku hiyo adhimu ya Kiswahili Duniani ambapo ni kufanya maadhimisho ya wiki nzima yaani tarehe 1 Hadi 7 Julai;

“Semina na makongamano ya ndani yatakayohusisha mada mbalimbali zinazohusu kiswahili, Kumbukizi za magwiji na wataalamu mbalimbali wa kiswahili, Siku maalumu ya Utamaduni wa mswahili, Kuenzi mchango wa waandishi wa vitabu mbalimbali vya kiswahili, Kughaniwa mashairi na tenzi mbalimbali, Maonesho ya vitabu na kazi za fasihi kwa ujumla”

Kaimu Katibu Mtendaji huyo aliongeza kuwa kutakuwa na Mijadala inayohusisha wanafunzi wa kiswahili katika ngazi vyuo vya kati na juu, Siku ya wahadhiri wa kiswahili, Siku ya kilele itahusisha Utoaji wa hotuba mbalimbali za viongozi , Utoaji wa tunzo mbalimbali zikiwamo za manguli wa ushairi, waandishi wa vitabu na waghani mashairi, Utoaji wa Makala mbalimbali na burudani mbalimbali.

Aliongeza kuwa siku hiyo ni Siku maalumu ya wanafunzi wa ngazi ya shule za msingi na sekondari ambapo kutakuwa na makala ya kuelekeza matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili pamoja na Utamaduni wake , kughani mashairi, nyimbo, ngoma na Sanaa mbalimbali za kiswahili.

Kiswahili kwa sasa kinatambulika miongoni mwa lugha rasmi katika Afrika hususani kwenye Bunge la Afrika , Umoja wa Frika, Jumuhiya ya Afrika Mashariki na Jumuhiya ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).