January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baga Friends yapongezwa kupanda SDL

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

WADAU wa soka Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wameipongeza timu ya Baga Friends ya Wilayani hapa kwa kifanikiwa kupanda Ligi Daraja la Pili (SDL) ngazi ya Taifa.

Timu hiyo iliyopambania nafasi hiyo kwenye michezo ya fainali uliyochezwa Lindi, ambapo timu ya Copco Veteran kutoka Mwanza walitwaa ubingwa baada ya kupaya ushindi wa goli 3-1.

Katika Ligi hiyo mchezaji wa Baga, Omary Killer alifanikiwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora, wakati tuzo ya Mfungaji Bora ikichukuliwa na John Masisilo, Temeke Squad ikitwaa tuzo ya Timu yenye Nidhamu huku ile ya kipa Bora ikienda kwa Mohamed Hussein wa Copco Veterans.

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Muharami Mkenge amesema kuwa, hatua hiyo ni ya faraja kwani tangu kuchaguliwa kwake timu hiyo imekuwa na mwenendo mzuri katika Ligi hiyo ya Mabingwa wa Mikoa.

“Ulipomalizika uchaguzi muda si mrefu ikaanza ligi mgazi ya Mkoa, ambapo hatua ya 16 bora ilifanyikia kwenye viwanja viwili, ambavyo ni hapa Mwanakalenge jimbo la Bagamoyo na wa shule ya Msongi Msoga Jimbo la Chalinze, timu ya Baga iliutwaa ubingwa wa Mkoa,” amesema Mkenge.

Amesema, hatua hiyo kwake aliipokea kwa faraja kubwa kwani inaonesha mwanga wa kwamba ubunge wake umekuja na matumaini mapta katika sekta mbalimbali ukianzia na mchezo wa soka.

“Timu yetu inaonesha kuimarika kadri inapocheza, ushuhuda huo unathibitishwa na namna ilivyokuwa inapambaana katika michezo yake, ukianzia Ligi ngazi ya Mkoa mpaka mabingwa wa Mikoa kisha kumaliza ikishika nafasi ya pili iliyowahakikishia kupanda Ligi Daraja la Pili Taifa,” amesema Mkenge.

Mmoja wa wadau wa soka Wilayani hapa, Karama Tamimu amesema, hatua hiyo ni faraja kwa wakazi wa Bagamoyo na Mkoa Pwani kwa ujumla kwani imeongeza idadi ya timu zinazoshiriki michuano iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Migui Tanzania (TFF).

“Nakumbuka tuna timu ya Rufiji United ya Rufiji, Stend Fc ya Bagamoyo na hii Baga Friend’s, niwaombe uongozi wa Mkoa uweke mipango mashubuti itayowawezesha timu hizo kufanya vizuri,” amesema Karama.