Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MATUKIO ya ukatili kwa watoto yamekuwa yakiendelea katika maeneo mbalimbali na kuchangia kufifisha ndoto zao.
Hali kama hii ndio iliyotokea miaka minne iliyopita kwa kijana moja wa kiume wa miaka 17 (jina tunalo) ambaye alijikuta analazimishwa kulawitiwa na mjomba wake.
Akisimulia mkasa huu kwa unyonge anasema “Nilikuwa namwamini sana na sikuwa na mashaka naye kwa vile ni njomba wangu. Sikutegemea kama angeweza kunitendea aliyonifanyia”
Kijana huyu anasema kwamba mjomba wake alimrubuni kwa kumpa pesa kila alipomuona na kumlaghai kwa maneno mazuri ya kumtaka aachane na tabia ya kukaa vijiweni.
Kijana huyo ambaye kesi yake ilikuwepo katika Mahakama ya Mkoa wa Kusini Unguja chini ya Hakimu Khamis Simai anasema kuwa alianza kukutana na hali hiyo tangu akiwa darasa la tisa .
“Kwa miaka mitatu alinifanyia vitendo hivi huku akiniambia nikisemaa atanifanyia kitu kibaya mimi na mama yangu “anasema.
Anaeleza kwama hali hii ilianza siku moja alipokuwa amekaa kijiweni na rafiki zake na kumwambia aende kumlimia migomba yake na atamlipa na kabla ya kufanya kazi hiyo alimpa shilingi Sh.10,000 na kumsii kuacha kukaaa kwenye vijiwe.
Anasema alikuwa akipokea pesa hizo na hakuwa na mashaka yoyote juu hasa kwa vile ni mjomba wake na kuona hakuwa na sababu za kumuuliza juu ya pesa hizo alizokuwa akimpa.
Mjomba wake aliendelea kumpa pesa mpaka siku moja akamuita na kumwambia amekuwa akimpa pesa hizo kwa madhumuni ya kuwa kumfanyia uovu.
Anasema baada ya kujua dhamira yake hiyo alianza kuzikataa pesa hizo,lakini siku moja alikutana naye njia wakati akirudi shule na kumchukuwa hadi kichakani.
Anaeleza baada ya hapo akawa anamfuata nyumbani kwao nyakati za usiku kabla ya siku moja kumuita nyumbani kwake na kumwambia akumne mwili wake.
Anasema kwamba wakati anamfuata nyumbani alikuwa akipita nyuma ya nyumba yao na kuanza kumfokea ni kwanini hakwenda wakati alipomuita.
“Ilikuwa mapema usiku na nilikuwa ninakula,mama alikuwa hayupo na alinilaumu tu na kuondoka huku akinisisitiza kwamba endapo nitasema atanifanyia kitu kibaya na mama yangu”, alisema.
Anasema aliogopa sana na akaanza kuja nyumbani majira ya saa 6 usiku ama saa 8 usiku kwa siku ambazo mama yake anakuwa hayupo.
Anasema kuwa mjomba wake aliendelea kumfanyia vitendo hivyo mpaka siku moja mama yake alipomuuliza na hapo ndipo alipochukua ujasiri na kusema ukweli.
Hata hivyo anasema baada ya mjomba wake kujuulikana aliacha kumfuata lakini alikuwa akijisifu na kusema kuwa hakuna kitu chochote kitakachofanyika juu yake na cha kushangaza imekuwa kweli maana kwa sasa mshitakiwa huyo yupo huru.
KAULI YA MAMA
Mama wa mtoto huyo anasema kuwa taarifa ya mtoto wake kufanyiwa vitendo hivyo alizipata kwa mwanawe wa kike ambae anaishi mjini ambaye alimueleza kuhusu mwenendo wa huyo mtoto.
Anasema baada ya kupata taarifa hiyo alirudi nyumbani na kumuita mwanawe na kumdadisi na alikiri kuwa kweli mjomba wake anamfanyia mambo mabaya.
“Niliposikia kauli hiyo tu nilianza kulia na kutoka na kwenda hadi kwa ndugu yangu huyo ambaye mimi na yeye bibi zetu ndugu ambapo tulishauriana kwenda Polisi,” anasema.
Anasema kuwa kesi ya mtoto huyo ilichukulia zaidi ya miaka mitatu hadi kumalizika kutokana na kubadilishiwa mahakimu kwa kila mara hadi hakimu Khamis Simai wa mahakama ya Mkoa Kusini Mwera alipohitimisha hukumu.
Jumla ya mahakimu watatu walisikiliza kesi hiyo akiwemo Mrajisi wa Mahakama Mohamed Ali Mohamed ambaye alikuwa hakimu wa mahakama ya Mkoa wa Kusini kabla ya kupata uteuzi huo, Haroub Sheh Pandu na kumalizia kwa Khamis Simai ambae alitoa hukumu wa kumuachia huru mshitakiwa kwa ushahidi wa shaka.
Mratibu wa masuala ya Wanawake na Watoto,Latifa Abdalla Maisara, anasema kuwa ni kweli kesi hiyo aliisimamia mpaka kufunguliwa kwake na kuonesha masikitiko yake kwa hukumu ambayo ilitolewa dhidi ya mshitakiwa huyo.
Bado kuna haja ya jamii kujenga utamaduni wa kutoa ushahidi wenye kushiba ili matendo haya watuhumiwa wake waweze kuchukuliwa hatua.
Unapotoa ushahidi wa kushiba inakuwa rahisi mtuhumiwa kutiwa hatiani, lakini pamoja na hilo na mahakama nazo zisiweke muda mrefu kesi hizi ambazo mwisho wake hutokea kama ambayo yametokea kwa kesi ya kijana huyu.
Hata hivyo kwa sasa kesi za aina hiyo itakuwa zinaenda kwa mwendo wa kasi baada ya kuwepo kwa Mahakama Maalumu ya udhalilishaji ambayo itakuwa na jukumu la kusikiliza kesi hizo tu.
Hatua hiyo inaonesha wazi kwamba itachangia watuhumiwa kutiwa hatiani na jamii kuwa na imani kubwa na washughulikiaji wa kesi hizo pamoja na Serikali yao.
Mara tu baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuapishwa aliagiza kuwepo kwa mahakama maaalumu ya udhalilishaji ili kuzifanya kesi hizo kwenda kwa haraka.
Tayari mahakama hiyo imeanzishwa Febuari mwaka huu, ambapo hivi karibuni mahakimu na waendesha mashtaka waliajiriwa maalumu kwa ajili ya kusimamia kesi hizo.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM