Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Ikiwa dunia ipo katika siku 16 za uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia, Chama cha Wafanyakazi wa viwanda, biashara, taasisi za fedha, huduma na ushauri (TUICO) kimeendelea kutoa elimu ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo mbalimbali ya kazi jijini Mwanza.
Akizungumza na chombo hiki, mkuu wa idara ya wanawake, watu wenye ulemavu, afya na usalama mahala pa kazi na mazingira TUICO, Bi. Maria Bange, amesema suala la ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi bado linahitaji juhudi za pamoja kwani jamii inalichukulia kama sehemu ya maisha.
“Asilimia kubwa ya wafanyakazi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Wengi wameona ni sehemu ya maisha katika sehemu za kazi. Lakini elimu zaidi inahitajika kwa wafanyakazi na waajiri ili wafahamu madhara ukatili na unyanyasaji,” amesema Bi. Maria
“Kwa nyakati tofauti tumefikia wafanyakazi 398 wa kiume na wa kike, vijana kwa wazee katika sehemu za kazi za Mwatex 2001 Ltd, Pamba Steel, Fanaka Fishnet (T) Ltd, Neelkanth Packaging Ltd, Sayona Drinks Ltd na MCL-Multi Cable Ltd. Mapokeo ya somo ni mazuri mno. Hii inaashiria uhalisia wa tatizo,” ameongeza Bi. Maria.
Naye Bi. Lulu Omary Zuberi, mtunza fedha katika kampuni ya MCL-Multi Cable Limited ya jijini Mwanza amesema MCL wamekuwa wakishughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia pale yanaporipotiwa lengo ni kuhakikisha kuna mazimgira rafiki ya kazi ambayo yana faida sio tu kwa wafanyakazi bali kwa mwajiri pia.
Baadhi ya wafanyakazi waliofikiwa na elimu ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia wamesema sio tu ukatili unasababisha maumivu kwa mtu mmoja bali unaathiri familia, uzalishaji na tija kazini sambamba na kuathiri maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla hivyo wametaka elimu kama hii iendelee kutolewa mara kwa mara na kwa makundi yote katika jamii ili kuutokomeza.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa