Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe.
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia mwanaume mmoja jina limehifadhiwa kwa sababu maalum za kipolisi ambaye ni Mkazi wa kijiji cha Kaloleni, wilayani Songwe akituhumiwa kumua Editha Msokwa (38) na mtoto wake mchanga wa miezi sita, Esther Emanuel.
Huku chanzo kikielezwa kuwa ni wivu wa mapenzi baada ya mtuhumiwa huyo kumtuhumu mkewe huyo kumzaa mtoto nje ya ndoa.
Mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mwambani, wilayani Songwe baada ya kujeruhiwa na wananchi, anadaiwa kumvizia mke wake akiwa amelala usiku na mtoto wake huyo wa miezi sita na kuwanyonga kabla ya kuuburuta mwili wa mkewe na kwenda kuuficha kwenye kibanda nje ya nyumba yao.
Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo , Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Septemba 24, 2023.
Amesema mtuhumiwa alikamatwa baada ya kuokolewa na viongozi wa kijiji chini ya Mwenyekiti Laiton Waya kutoka katika kundi la wananchi wenye hasira kali waliomkamata mara baada ya kufanya tukio hilo la mauaji ya kinyama na kuanza kumshushia kipigo kigali.
“Mtuhumiwa huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mwambani akiwa chini ya ulinzi na uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi unaonesha kuwa mtuhumiwa kabla ya kutekeleza mauaji hayo walikuwa na mgogoro na mke wake akimtuhumu kuzaa nje ya ndoa,” alifafanua Kaimu Kamanda Ngonyani.
Aidha, Kaimu Kamanda Ngonyani amesema kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na pindi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
More Stories
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia