November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AzamTV yazindua ofisi Kanda ya Kaskazini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Arusha

WATEJA na wadau wa AzamTV Kanda ya Kaskazini kuanzia jana (Februari 1,2022) wameanza kupata huduma kwa ukaribu zaidi kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji.

Hayo yamesemwa jana Afisa Mtendaji Mkuu wa AzamTV Limited, Sabrina Mohamedali, wakati wa uzinduzi wa ofisi ya Azam TV Kanda ya Kaskazini hafla ambayo imefanyika mkoani Arusha.

Mohamedali amesema; “AZAMTV tumeamua kusogeza huduma zetu Kanda ya Kaskazini kuanzia Februari 1, mwaka huu ambapo wateja na wadau wetu watapata huduma za AZAMTV kwenye ofisi zetu za kanda zilizopo hapa Arusha, Summit Centre Barabara ya Sokoine.”

Ametaja huduma zinazopatikana kuwa ni mauzo ya visimbuzi vya antenna, dish na camcard, matengenezo ya visimbuzi na kuunganishwa na huduma ya AzamTV Max.

“Pamoja na huduma hizi, AzamTV kwa kushirikiana na washirika wetu Sunking na Engie Mobisol Solar kwa pamoja tuna huduma ya camcard ambayo mteja anaweza kufanya malipo ya kidogo kidogo kupitia mitambo yao ya solar na TV,” amesema Mohamedali na kuongeza;

Afisa Mtendaji Mkuu wa AzamTV Limited, Sabrina Mohamedali, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Ofisi za AzamTV Kanda ya Kaskazini, ambapo hafla hiyo ilifanyika jijini Arusha,jana.

“Dhamira yetu ni kusogeza huduma karibu, kwa sasa tumeanza na Kanda ya Kaskazini tukiwa na lengo la kuzikifikia kanda zote Tanzania.”

Amesema kama ilivyo kauli mbiu yao; “Burudani kwa wote’ tunadhihirisha hili kwa kuendelea kuwafikia wateja na wadau wetu wote.”

Amewashukuru mawakala wao wote waliopo Arusha kwa mchango wao mkubwa kwa kutoa huduma kwa wateja wao. Mawakala hao ni Chuwa Electronics, Leo Investment, Patel Shop, Sunlight power supplies na Benson & Company Ltd