Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MSAFARA wa viongozi sita wa benchi la ufundi na wachezaji 25 wa klabu ya Azam FC jana usiku wamewasili salama jijini Dodoma huku wakiwa wamepania kuchukua alama zote sita katika mechi zao mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Azam itatupa karata yake ya kwanza Aprili 16 kuvaana na Maafande wa JKT Tanzania katika mchezo utakaochezwa saa 8:00 mchana lakini watarudi tena dimbani Aprili 22 kuvaana na Dodoma Jiji FC.
Itakumbukwa kuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Oktoba 30 Azam walilazimishwa sare ya goli 1-1 na Maafande hao na Novemba 5 waliibuka na ushindi mnono wa goli 3-0 dhidi ya Dodoma.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema kuwa, mechi hizo mbili ni muhimu sana kwao kwani wanachohitaji ni kupata matokeo mazuri ili kuendeleza makali yao katika Ligi.
Ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Ihefu na ule wa 2-0 walioupata katika mchezo wao uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar unawapa morali kuelekea kwenye mechi hizo ambazo wanahitaji kuvuna alama zote sita ambazo zitawarejesha kwenye mikakati waliyokuwa nayo mwanzo wa msimu.
Zaka amesema kuwa, hawana wasiwasi wowote katika mchezo huo kwani wana historia nzuri na uwanja huo kwani mwaka 2008 wakati wanapanda Daraja walikuwa katika kituo cha Dodoma na hawajawahi kupoteza mchezo zaidi ya ushindi na sare.
“Ukiacha Azam Complex, Chamazi nyumbani kwetu kwa pili ni Dodoma hivyo tutakuwa katika uwanja ambao tumeuzoea hivyo tunawaahidi raha wakazi wa Dodoma pamoja na mashabiki wetu wote,” amesema Zaka.
Amesema, kikosi kinachoondoka kinaundwa na Wilbol Maseke, Benedict Haule, Mathias Kigonya, Braison Rafael, Prince Dube, Nico Wadada, Abdul Haji Omar ‘Hamahama’, Bruce Kangwa, Paschal Msindo, Mudathir Yahya, Obrey Chirwa, Never Tigere na Danny Amoah.
Wengine ni Abdallah Kheri Sebo, Ally Niyonzima, Idd Suleiman Nado, Awesu Ally Awesu, Ayoub Lyanga, Yakubu Mohamed, Ismail Aziz Kader, Agrey Morris, Mpiana Monzinzi, Emmanuel Kabelege, Yahya Zayd na Salum Abubakary ‘Sure Boy’.
Alisema, katika mchezo huo watawakosa Emmanuel Charles na kiungo mshambuliaji Khleffin Hamdoun ambao ni majeruhi huku mshambuliaji Prince Dube akikosa mchezo wa kwanza baada ya kupata kadi tatu za njano.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025