Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Asasi mbalimbali za kiraia na taasisi zisizo za Serikali zimetajwa kuwa na mchango katika ukuzaji wa tasnia ya uvuvi mdogo nchini na Afrika kwa ujumla.
Hayo yamesemwa,Desemba 05, 2024 jijini Dar-es-Salaam na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) Saleh Yahya wakati akifungua warsha iliyoandaliwa na Kamisheni ya Bahari ya Hindi kupitia mradi wake wa EcoFish,iliolenga kuangazia mchango wa taasisi hizo katika kukuza tasnia ya uvuvi mdogo kwa mataifa wanachama wa Kamisheni hiyo ikiwa ni pamoja na Tanzania.
“Sisi kama Tanzania kupitia Warsha hii tumejifunza namna ambavyo wadau wa sekta binafsi wanaweza kutusaidia kuendeleza Uvuvi Mdogo ambao kama mnavyojua unajumuisha takribani asilimia 90 ya Shughuli za Uvuvi unaofanyika nchini kwa ujumla” Ameongeza Bw. Yahya.
Kwa upande wake Ofisa Mfawidhi kutoka Kamisheni ya Bahari ya Hindi (IOC), Marc Maminiana,amesema kuwa warsha hiyo itawapa taswira ya namna ya kuunganisha majukumu ya taasisi hizo, zisizo za Serikali ili ziweze kuwa na tija na kuwa daraja kwa jamii ya wavuvi wadogo na Serikali.
Akizungumzia manufaa ya warsha hiyo mwakilishi wa Shirika lisilo la Serikali la “CARDIO” kutoka Kenya Benedict Kiilu amesema kuwa, matokeo ya warsha hiyo kwao ni pamoja na kuwasaidia kufanya shughuli zao kwa uwazi na kupitia ushirikiano watakaokuwa nao kuanzia sasa itawasaidia kuepuka kutekeleza miradi inayofanana kwenye jamii wanazozihudumia.
Pamoja na mambo mengine warsha hiyo imepokea na kujadili taarifa ya Mshauri Mwelekezi aliyefanya utafiti wa mchango wa taasisi zisizo za Serikali kwenye sekta ya uvuvi kwa mataifa yanayotekeleza miradi iliyopo chini ya Kamisheni ya Bahari ya Hindi (IOC).
More Stories
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba