December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso:Boti za kisasa zitachochea maendeleo,Pangani, Zanzibar

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

Wakazi wa Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara,wanalazimika kusafiri hadi jijini Dar-es-Salaam,wakiwa wanataka kwenda Zanzibar.Hivyo ili kutatua changamoto hiyo,zinahitajika boti za kisasa zitakazofanya safari kati ya Wilaya ya Pangani na Visiwa vya Zanzibar.

Boti hizo zitarahisisha usafiri kwa wakazi wa mikoa hiyo,na kuchochea uchumi wa Wilaya ya Pangani kupitia utalii kutokana na uwepo wa mbuga ya Saadan.

Akisisitiza jambo hilo,Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani Jumaa Aweso, ameiomba serikalli kuwapatia boti hizo za kisasa na zenye kasi katika wilaya hiyo.

Aweso ametoa ombi hilo, katika kikao cha ndani cha Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Hemed Suleiman Abdullah na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM),wilayani Pangani mkoani Tanga.

Amesema,miongoni mwa mahitaji ya watu wa Pangani,ni upatikanaji wa boti hizo za kisasa, ambazo zitachochea kasi ya maendeleo kati ya Zanzibar, Pangani na maeneo mengine.

“Jiografia ya Pangani inafanana na Zanzibar,lakini pia Wilaya ya Pangani ina mbuga ya Saadan.Ninyi Zanzibar mna utalii mkubwa lakini hamna mbuga.Kwa namna Wilaya yetu ivyokaa ipo karibu na Mombasa, Tanga Mjini, Muheza, Handeni,Kilindi na Wilaya zingine, lakini pia tuna Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha na Manyara leo mtu akitaka kwenda Zanzibar hadi aende Dar-es-Salaam wakati njia ya hapa ni karibu,” ameeleza Aweso na kuongeza:

“Tukipata “Fast boat” hapa maana yake watalii mchana wataweza kutembelea Pangani, jioni wakarudi Zanzibar, hii itaifungua Pangani kiuchumi,”.

Akijibu ombi hilo,Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah,amesema wapo katika hatua za mwisho za mchakato wa manunuzi ya boti mpya mbili za kisasa zinazokwenda kasi, zitakazofanya safari kati ya Tanga, Pemba, Unguja, Dar-es- Salaam na Mombasa nchini Kenya.

Makamu wa Rais Abdullah amesema, uundwaji wa boti hizo utakamilika miezi mitatu ijayo, na zitafungua njia zaidi za uchumi kati ya Zanzibar na maeneo zitakapo fanya safari ikiwemo Tanga.

Amesema,boti hizo zikiwasili na kuanza kufanya kazi, atashirikisha adhima ya Mbunge Aweso ya kuhitaji kuwe na safari za kupitia Pangani.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajab Abrahaman Abdallah amesema, serikali imepeleka miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa huo, ikiwemo sekta ya afya,elimu, barabara,maji na umeme.

“Mkoa wa Tanga tuna vijiji 779,ambavyo vyote vimeisha pelekewa umeme kwenye.Lakini Pangani tuna umeme kwenye vijiji vyote 33, vilevile Handeni, Lushoto, Mkinga, Muheza na Kilindi pia kuna umeme,”.