-Amezindua bodi ya saba ya Bonde la Maji Ziwa Victoria
-Amezindua nembo na jengo la ofisi ya Bonde la Maji Ziwa Victoria
Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameziagiza Bodi za maji nchini kuwachukulia hatua watu wanaochimba visima bila vibali,wanaofanya shughuli mbalimbali katika vyanzo vya maji pamoja na wanaotumia maji bila vibali.
Waziri Aweso ametoa maagizo hayo leo jijini Mwanza wakati akizindua Bodi ya saba ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB),nembo na jengo la ofisi ya bodi hiyo, uliofanyika katika ofisi za bonde hilo iliopo mkoani Mwanza.
“Tunatambua maji ni uhai,bidhaa kiuchumi hayana mbadala,wajibu wetu kuhakikisha tunalinda,tunatunza na tunahifadhi vyanzo vya maji kwa maendeleo hivyo naagiza bodi za maji nchini kuhakikisha zinasimamia sheria na kuchukua hatua kwa wale wote wanaovunja sheria”amesisitiza Aweso.
Pia amewaagiza Wakurugenzi wa mabonde yote kuendelea kuboresha mifumo wa ukusanyaji na uchakataji wa takwimu za rasilimali za maji kwa kuwa ni uti wa mgongo wa usimamizi wa rasilimali za maji.
“Ofisi ya Bodi ya Bonde litunzwe ili liweze kutumika kwa muda mrefu,nimepitishwa katika mfumo wa ukusanyaji na uchakataji wa takwimu za rasilimali za maji nimeona kazi kubwa ilifanyika katika eneo hili nimefurahishwa na jitihada zinazoendelea katika kuboresha takwimu kwa lengo la kupata hisibati,”.
Aidha Waziri Aweso ameielekeza Bodi ya saba ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), kuhakikisha watumiaji wa maji wanalipa ada za matumizi ya maji kwa wakati, kutoa vibali vya matumizi ya maji kwa wakati, kusimamia ukamilishaji wa mchakato wa kuwa na mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji na kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, kubuni mikakati itakayowezesha kuongeza mapato ya bodi, kununua magari na vitendea kazi vinavyohotajika.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Sita ya Bonde la Ziwa Victoria Magreth Musiba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo,ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wao walipata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuandaa na kuteketeza mpango mkakati wa kuongeza mapato ambapo bodi ikifanikiwa kuongeza mapato kutoka milioni 600 mwaka 2018 Hadi kufikia bilioni 3.7 mwaka 2021.
Bodi imewezeshwa uundwaji wa jumuiya 14 za watumia maji na kuzijengea uwezo, ujenzi na ukarabati wa vituo 28 vya kufuatilia mwenendo wa maji, Kuandaa mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji (IWRMDP) ambao mchakato wake umefikia asilimia 40, huku ikifanikiwa kutambua vyanzo 157 na kuweka mipaka ya kudumu kwenye vyanzo 14 vya maji huku ikikarabati bwawa 1 lenye ujazo wa lita milioni 90 na kuchimba visima virefu 35 na kati ya hivyo visima 20 vimewekewa miundombinu na wananchi wananufaika na huduma ya maji.
“Bodi inakabiliwa na changamoto za uharibufu wa vyanzo vya maji unaotokana na shughuli za kibinadamu,vitendea kazi vichache visivyotosheleza mahitaji kama vile magari,vifaa vya kufuatilia hali ya maji ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi pia baadhi ya watumia maji kutokuwa na utayari wa kulipa ada za matumizi ya maji kwa wakati au wengine kutokulipa kabisa,”ameeleza Musiba.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli, ameeleza kuwa lazima Sheria isimamiwe vizuri ambapo Mkoa wa Mwanza una Wilaya saba kati ya hizo sita zimezungukwa na Ziwa Victoria hivyo wanakila sababu ya kulitunza kwani Kanda ya Ziwa wanategemea uchumi kupita Ziwa Victoria.
Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji nchini, Dkt.George Lugomela,ameeleza kuwa wizara ya maji kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 imepanga kujenga mabwawa 20 ya utunzaji wa rasilimali za maji.
Maji yanaweza kuisha hivyo ni lazima yatunzwe na kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na kila bonde nchini linatakiwa kuandaa mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezwaji wa rasilimali za maji.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini