Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Waziri wa Maji Jumaa Aweso,amefanikisha utekelezaji wa mradi wa maji wa dharura Buhongwa,ndani ya siku moja uliokuwa unapaswa kukamilika ndani ya siku saba,baada ya Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA), kutekeleza agizo lake la kufanya kazi usiku na mchana na kuongeza nguvu kazi ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Ambapo Septemba,8,2024,Aweso,baada ya kutoa maagizo kwa MWAUWASA,majira ya mchana wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Buhongwa na Lwahima,katika kituo cha kusukuma maji Sahwa,jijini Mwanza.Aliweka kambi katika eneo hilo na kushuhudia mafundi wakifanya kazi ya ulazaji wa bomba la inchi 12 lenye urefu wa Kilomita 4.5 kutoka tenki la maji Sahwa kwenda eneo la Buhongwa Center.
Hata hivyo jitihada za mafundi hao zilizaa matunda majira ya saa tano na nusu usiku na Waziri huyo wa Maji,aliwasha mtambo rasmi wa kusukuma maji ambayo yalifika kwenye maunganisho Buhongwa Center na kushuhudia na baadhi ya wananchi wa maeneo hayo.
Akizungumza mara baada ya kuwasha mtambo huo,Aweso, ameeleza kuwa eneo la Buhongwa lilikuwa na changamoto ya maji,wametembelea na kuona hali halisi, lakini walitoa maelekezo kwamba Wizara ya Maji,lazima ifanye kazi kama jeshi,usiku,mchana na kukesha lakini maji yafike Buhongwa Center.
Pia ameitaka MWAUWASA kuhakikisha inasambaza maji hayo ndani ya siku saba pamoja na kufuata utaratibu wa kuwaunganishia wananchi maji.
“Haya ndio maelekezo, kiongozi anapo toa ni kuhakikisha jambo linatokea,maji mliokuwa mnahangaika kwa muda mrefu sasa tumeisha yafikisha ‘centre’.Jukumu lenu ni kuhakikisha haya maji yanasambazwa,katika mitaa mbalimbali na mkisha yasambaza muunganishie watu maji kwenye nyumba zao ili waweze kufurahia,” ameeleza Aweso na kuongeza:
“Tunajua watu wataomba maunganisho ya maji,yasizidi siku saba.Mtu akiomba kuunganishiwa maji aunganishiwe,siyo mpaka atoe kitu kidogo ndio apate, hapana, utaratibu ufuatwe kuhakikisha watu wanapata maji safi na salama,”.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Nelly Msuya, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso,amesema lengo la mradi huo ni kuboresha mtandao wa maji.Hivyo utakwenda kutatua changamoto ya maji kwa wananchi hao,ambao unagharimu kiasi cha milioni 864,fedha kutoka wizarani ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha wastani wa lita za maji milioni 8.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria