November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso aitaka Kashwasa kulipa deni la umeme

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Waziri wa Maji Juma Aweso ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga(Kashwasa) kulipa madeni yake ya umeme kwa wakati pamoja na kununua vipuli na dawa kwa ajili ya mitambo ya maji.

Aweso ametoa agizo hilo Januari 8,2024,wakati alipotembelea mradi wa maji wa Ihelele uliopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

Pia ameitaka mamlaka hiyo kuendelea na mpango maalumu wa kuuza maji mengi zaidi kwa mamlaka za maji zitakazokuwa zinahitaji.

Sanjari na hayo Aweso ametumia fursa hiyo kueleza kuwa hatovumilia Mkurugenzi wa Mamlaka yoyote ya maji ambae atakuwa mvivu katika utendaji kazi.

Hivyo amewataka wakurugenzi wa Mamlaka hizo za maji nchini kujitathimini na kufanya kazi kwa bidii ili kuepuka tabia ya kuwa na visingizio katika utendaji kazi.

“Kumekuwa na visingizo vingi sana kutoka kwa wakurugenzi hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji,mkurugenzi ambae hataweza kwenda na kasi ya utendaji kazi ni bora aniandikie barua ya kujiuzulu mapema,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga(Kashwasa) Patrick Nzamba amesema mamlaka hiyo hadi kufikia Desemba 31,2023 ilikuwa inadai kiasi cha bilioni 14 kwa wateja wake wa mamlaka za maji.

Amesema wanakabiliwa na changamoto kubwa sana ya deni la umeme katika kuendesha mitambo yake ya kuzalisha maji katika mradi wa Ihelele ambapo kwa mwezi wanatumia kiasi cha milioni 650.

Nzamba amesema ongezeko la matope katika mfumo wa kutibia maji kumesababisha viwango vya kuzalisha maji kwa siku kupungua kutoka lita za ujazo 69,000 mpaka 26,000.