December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso aishukuru WHO ushirikiano na Serikali

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake mzuri na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji.

Alitoa shukrani hizo wakati akifunga mafunzo ya wiki tisa yaliyofadhiliwa na Benki ya Dunia ya kuzijengea uwezo Mamlaka za Maji ili kuwa na sifa ya kupata Mikopo kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ya fedha, kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya Sekta ya Maji nchini.

Alisema, mafunzo hayo yalihusisha idadi ya Wataalam 40 kutoka Sekta ya Maji na yamewawezesha kuwa na uwezo na mbinu mpya za ushawishi kwa taasisi za fedha ikiwemo uandishi bora wa maandiko na usimamizi wa miradi, kupunguza upotevu wa maji, kupanga mipango bora na endelevu, kukusanya mapato na hatua mbalimbali ambazo zitawezesha maendeleo ya sekta ya maji na hivyo kuondoa utegemezi wa fedha kutoka Serikalini.

Alisema Benki ya Dunia imekuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya sekta ya maji ikiwemo miradi ya maji ambayo inatekelelezwa kupitia Program ya Lipa Kutokana na Matokeo (PfoR).

Aidha, alilomba Benki hiyo kupanua wigo wa mpango wa PfoR ili uweze kusaidia maendeleo ya Sekta ya Maji katika Mamlaka za Maji nchini ambapo programu hiyo inagusa zaidi miradi ya maji ya vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia , Tanzania, Ruth Kennedy Walker aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushikiano mkubwa katika kazi mbalimbali hususan katika Sekta ya Maji.

Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwapa wigo mpana wa kupata fedha katika vyanzo mbalimbali vya fedha ambapo Benki za Biashara ndiyo watoaji wakubwa wa fedha za mikopo ila huitaji andiko lenye ushawishi.

Kwa upande wake Mhandisi Humphrey Mwiyombela ambaye ni mmoja wa washiriki waliopata mafunzo hayo alisema mafunzo yamekuja katika muda muafaka ambapo Wizara ya Maji inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Tatu (WSDP III) ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.

Mafunzo hayo yamewezesha kushirikishana uzoefu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo utatuzi wa migogoro katika maeneo ya kazi, kupunguza upotevu wa maji na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji, pia kuzingatia gharama.