April 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askofu Masondole awataka vijana kutofuata mila na desturi zisizokubalika nchini

Fresha Kinasa, TimesMajira Online Mara.

MHASHAMU Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda Simon Chibuga Masondole amewataka Vijana walioko katika shule za Sekondari, Vyuo na Taasisi mbalimbali za elimu nchini kutojaribi kujiingiza katika mila na desturi zisizokubalika hapa nchini ikiwemo ushoga na usagaji kwani kufanya hivyo ni kuharibu utu wao na thamani yao.

Amesema,mambo hayo hayafai kwa namna yoyote lazima yakemewe vikali na msisitizo wa maadili mema uendelee kutolewa.Sambamba na mafundisho ya kiroho yatakayowajenga wapende  kumtumikia Mungu kwa moyo na akili zao zote  na kuachana na maisha ya kutamani kutenda dhambi.

Askofu huyo ameyasema hayo Machi 4, 2025 wakati wa adhimisho la  Misa takatifu ambapo pia katika misa hiyo   ametoa sakaramenti ya Kipaimara kwa Waumini wa Kigango cha Mtakatifu Yohana Mbatizaji Senta ya Kurusanga Wilayani ya Bunda ambayo ilihudhuriwa Waamini wa kanisa hilo na Wanafunzi wa shule za  Sekondari ambao ni Wakatoliki.

“Niwaombe Vijana ,  someni kwa bidii na kumtangiliza Mungu katika masomo yenu. Epukaneni na mila mbaya ambazo baadhi ya Mataifa ya nje wanafanya huko kwao na kutaka kutuletea huku. Ushoga na usagaji vitendo hivyo ni ujinga lazima viepukwe  kabisa iwe vyuoni ama shuleni hakikisheni mnavipinga. Vitendo hivyo ni chukizo kubwa  mbele za Mungu, zipo mila nzuri ambazo mnapaswa kuzifuata zenye kulinda utu,   heshima na hadhi yenu na mkasaidia Jamii katika mambo mazuri. ” amesema Askofu Masondole.

Pia, amewataka Wazazi na walezi kuimarisha malezi kwa watoto wao na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo havifai kisheria na Mbele za Mungu  Sambamba na kuwalea Watoto katika misingi ya imani na kuhakikisha wanasoma kwa faida yao, Jamii na Taifa pia. 

“Mila na desturi zetu ambazo ni mbaya tunapaswa  kuziacha, mfano ukatili wa  kuoneana oneana,  kupigana pigana kwa mapanga   kufanya hivyo ni  kuwavuta  wengine waje  kwa Kristo.”amesema Askofu.

“Wakristo tunapaswa kuishi kwa upendo na umoja kwa kumfuata Kristo ambaye ni kielelezo chetu.  Tuachane na matendo maovu yasiyofaa bali tutende matendo mema  yanayokubalika katika Jamii yetu. Maisha ya hapa duniani ni ya mpito yaani ni zawadi tu  tunapita, lazima tukazanie maisha ya umilele.” amesema.

Kwa upande wake Joyce Petro Mkazi wa Kurusanga amesema Wazazi na walezi wanalojukumu la kuzungumza na watoto wao kuwaeleza mambo yasiyofaa na mambo yanayofaaa ili kuwajengea uelewa utakaowafanya wajitambue.