December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askofu aunga mkono mpango wa Rais Samia

*Ni wa kutaka kufunga kamera barabarani kudhibiti rushwa kwa
trafiki hapa nchini, kuimarisha usalama, ashauri elimu kwanza

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, ampongezwa kwa dhamira yake ya kutaka kufunga kamera barabarani ili kukabiliana na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya trafiki pamoja na kuimarisha usalama.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashehe ya Maadili Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga, jana jijini Dar es Salaam na kusisitiza kwamba dhamira hiyo italeta mabadiliko ya kiusalama na kupambana na rushwa kwa trafiki.

“Nampongeza Rais Samia kwa kutaka kuleta mabadiliko makubwa ya teknolojia barabara, lakini namshauri zoezi hilo litanguliwe na elimu kwanza, kwani wananchi hawana uelewa wa kutosha.

Tunaona hata matumizi ya taa za barabarani bado ni tatizo kubwa kwa jiji la Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Morogoro ni vema kwenye miji hiyo zichaguliwe baadhi ya barabara ili ziwa darasa la la kuanza kutumika teknolojia hiyo,” amesema.

Amesema baadhi ya madereva jijini Dar Salaam wamekubaliana na Askofu Mwamalanga wakitaka ianze kutolewa elimu kwa vitendo, kabla ya kuanza kufungwa kwa kamera hizo.

“Tunaiunga mkono kauli ya Rais Samia kufunga kamera barabara, uamuzi huo utakomesha vitendo vya rushwa barabarani kama elimu itatangulia,” amesema Askofu Mwamalanga.

Mwishoni mwa wiki wakati akiapisha viongozi aliowateua, Rais Samia alisisitiza dhamira yake ya kufunga kamera barabarani ili kupambana na vitendo vya rushwa.

Kabla ya hapo, Agosti 25, 2021 Rais Samia, aliagiza Jeshi la Polisi kukomesha tabia za baadhi ya askari wake hususan wa Usalama Barabarini kupokea rushwa kwenye magari.

“Wakati mwingine ni vigumu kubadilisha tabia, lakini inaweza kurekebishika kukiwa na teknolojia inayolazimisha watu wafuate teknolojia inavyotaka.

Mfano tukiweka kamera za barabarani hakutakuwa na sababu ya askari kusimama barabarani kusimamisha magari, teknolojia itatoa mwongozo wa kila kitu na rushwa haitakuwepo,” alisema.

Rais Samia alifafanua kuwa uwekezaji huo ukifanyika kwenye teknolojia utasaidia kupunguza idadi ya askari barabarani, hivyo watakwenda kwenye maeneo mengine yenye uhitaji.

Matamanio ya Rais Samia wa kutaka kufunga kamera kunaungwa mkono na wananchi mbalimbali waliotoa maoni yao mitandaoni kuhusiana na kauli hiyo ya Rais.

Aidha, aliweka wazi kwamba zipo video fupi ‘video clips’ nyingi ambazo zimekuwa zikizunguka ndani na nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii zikionesha baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi hususan matrafiki wakiomba na kupokea rushwa kwenye magari.