February 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askari watatu wa TANAPA wafukuzwa kazi kwa tuhuma za rushwa

Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online,Bukoba

Askari watatu wa Jeshi la Hifadhi ya Taifa ( TANAPA ) wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa, kisha kuruhusu ng’ombe kuchungwa ndani ya hifadhi kinyume na sheria.

Hayo yamebainishwa Februari 11,2025 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU )Mkoa wa Kagera,Vangsada Mkalimoto, wakati akiongea na vyombo mbalimbali vya habari mkoani humo.

Mkalimoto,amesema walipokea taarifa ikihusisha Askari 13 katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi -Chato,wilayani Biharamulo mkoani Kagera, wakituhumiwa kuomba na kupokea rushwa na kuruhusu ng’ombe )kuchungwa ndani ya hifadhi hiyo kinyume na sheria na uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini ukweli wa taarifa hiyo.

Amesema watuhumiwa hao wamefikishwa katika Kamati ya Uchunguzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Burigi-Chato, ambapo ushahidi ulitolewa mbele ya kamati hiyo na watuhumiwa wote 13,wamepatikana na hatia hivyo wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu.

Kati yao Askari 3 wamefukuzwa kazi,4 wameshushwa vyeo na 6 wamepunguziwa mshahara kwa asilimia 15 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Sanjari na hayo amesema TAKUKURU wanaendelea kupambana na kuzuia vitendo vya rushwa katika sekta zote, ili kuhakikisha ustawi wa nchi,hivyo amewataka watumishi wote wa umma kuzingatia maadili ya kazi zao.