March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 98.7, ya watoto Ilemela wamepata huduma ya matone ya Vitamini ‘A’

Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza 

 Zaidi ya watoto 77,000 wenye umri wa miezi sita hadi miezi 59,wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,wamepatiwa huduma ya  matone ya Vitamini A,dawa kinga za minyoo pamoja na upimaji wa hali ya lishe katika kipindi cha mwezi mmoja.

Huduma hiyo imetolewa na Halmashauri hiyo kupitia kampeni ya kitaifa ya utoaji wa matone ya Vitamini A ,dawa kinga za minyoo  sambamba na upimaji wa hali ya lishe kwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi 06 hadi miezi 59.

Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF ya mwaka 2018 imebainisha kuwa Vitamin A huimarisha mfumo wa kinga kwa mtoto na kumuepusha na magonjwa hatari kama vile surua na kuhara.Hivyo dozi mbili za matone ya vitamin A za kila mwaka zinaweza kuokoa maisha  ya maelfu ya watoto.

Kampeni ya utoaji wa matone ya Vitamin A chini ya kauli mbiu, “Matone ya Vitamin A ni muhimu kwa ukuaji wa maendeleo ya mtoto;tumfikie kila mtoto popote alipo” ilianza Juni 01 na inatarajiwa kukamilika Juni 30,2025.

Akizungumza wakati  alipotembelea vituo  vya kutolea huduma za afya katika zahanati ya Nyakato na kituo cha afya cha Buzuruga,Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Manispaa Ilemela,Pili Kassim, amesema, katika kampeni hiyo lengo lilikuwa ni kuwafikia watoto 78,406,lakini hadi kufikia Juni 26,2025,wametoa huduma kwa watoto 77,412 sawa na 98.7.

“Tunatarajia kwa muitikio huu wa wazazi hadi kufikia mwisho wa kampeni hii tutakuwa tumevuka malengo”, amesema  Pilli.

Pia  ametaja faida za matone ya Vitamin ‘A’,kuwa ni  kuwakinga na kuwaepusha na maradhi mbalimbali yanayatokana na ukosefu wa  vitamini hiyo mwilini, kuimarisha uono kwa watoto na kuongeza damu.

Kwa upande wao  wananchi wa Kata ya Buzuruga,Hawa Masinde Silima na  Judith Mzingu, miongoni  mwa wazazi waliofika kituo cha afya Buzuruga kwa ajili ya watoto wao kupatiwa huduma ya matone ya vitamini ‘A’, wamewahimiza wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao kupatiwa huduma hiyo wawapeleke kwani huduma hiyo inatolewa bure kwenye vituo vya afya.

Naye Juliana Methew mkazi wa kata ya Nyakato,ametoa wito kwa kina baba kushirikiana na wenza wao kusimamia afya na ustawi wa watoto.