* Waliohama kupokelewa vijiji jirani, waipongeza Serikali
Na Beatus Maganja, Timesmajira Online,Malinyi.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi,Sebastian Waryuba amesema zoezi la kuwalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo kilichopo ndani ya Pori la Akiba Kilombero mkoani Morogoro linaendelea vizuri.
Ambapo asilimia 93,tayari wamekwishalipwa fidia zao kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi katika Hifadhi hiyo na asilimia 7 ya wananchi waliosalia wanaendelea kushughulikiwa ili kukamilisha malipo yao.
Akizungumzia zoezi hilo Desemba 31, 2024 wilayani humo,Sebastian amesema Serikali imetoa zaidi ya billioni 6.9,kwa ajili ya kulipa wananchi 1,056, ili waweze kuhama kwa hiari kutoka maeneo ya hifadhi huku akitoa maelekezo kwa Watendaji wa Vijiji 32 wilayani Malinyi kuwapokea ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.
“Si kweli kwamba wananchi wa Ngombo hatujawaambia mahali pakwenda,katika barua yangu ya tarehe 4 Desemba, 2024 niliyowaandikia watendaji wa vijiji 32 vilivyo ndani ya Wilaya ya Malinyi, nilitoa maelekezo ya kuwapokea wananchi wa kijiji hicho wanaopisha shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Kilombero, na ndivyo inavyofanyika na pia nilielekeza watendaji hao wawataarifu wananchi wote kupitia mikutano ya hadhara,” amesema na kuongeza:
“Tangu wananchi wangu wa Ngombo walipoanza kuhama kwenda katika maeneo hayo sijapata malalamiko yoyote kwa simu au kwa mdomo, kwamba wamezuiliwa kukaa mahali fulani na kwa taarifa nilizonazo baadhi yao wamehamia sehemu mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Lindi, Ruvuma, Pwani na Halmashauri ya Mlimba.Naamini mambo yanakwenda vizuri na ndivyo ilivyo,”.
Kuhusu wanafunzi waliokuwa wanasoma shule katika Kijiji cha Ngombo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema amekwishatoa maelekezo kwa Ofisa Elimu kuwapokea na kuwasajili katika shule zilizopo kwenye vijiji vilivyo ndani ya Wilaya hiyo bila masharti yoyote ili waweze kusoma kwa uhuru.
Sanjari na hayo amesema, wananchi wa Kijiji cha Ngombo waliandaliwa mapema kwa kupewa elimu juu ya malipo ya fidia ili weweze kuhama kutoka katika eneo la Hifadhi ya Kilombero tangu Agosti, 2024. Hivyo, walikuwa na uelewa kuhusu zoezi hilo na amewataka kuepuka watu wenye nia ovu ya kupotosha dhamira njema ya zoezi hilo.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Biro Elizabeth Mnenuka amekiri kupokea zaidi ya wananchi 50 katika Kijiji cha Biro na wengine zaidi ya 30 katika Kijiji cha Mbalinyi na kuongeza kuwa baadhi yao tayari wameshapatiwa maeneo kwa ajili ya kuendeleza kwa kilimo na makazi.
Nao wananchi waliohamia Kijiji cha Biro kutoka Kijiji cha Ngombo wameishukuru Serikali kwa kuwalipa fidia zao kwa wakati ambazo zimewasaidia kuhama na kuanza maisha mapya katika vijiji jirani.
“Toka nitoke Kijiji cha Ngombo ambapo tuliondolewa kisheria kwakweli sina changamoto yoyote kimaisha, niko vizuri naishi vizuri na familia. Naishukuru Serikali, fidia nimepata mpaka hapa sina neno na Serikali,” amesema Daudi Lyambu
Ikumbukwe kuwa mnamo Februari 17, 2023 Pori la Akiba Kilombero lenye sehemu A na B lilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 64 kufuatia kupandishwa hadhi kwa sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero kuwa Pori la Akiba.
Aidha, kufuatia kuanzishwa kwa Pori la Akiba Kilombero, masharti na sheria zinazosimamia eneo hilo zilibadilika ambapo shughuli zote za kibinadamu zimesitishwa isipokuwa zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria.
Lengo la Serikali likiwa ni kuimarisha usimamizi wa eneo hilo kwa kuhifadhi vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori ili kuongeza tija ikiwemo upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Mwl. Nyerere.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024