Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga,imefanya ukaguzi wa leseni za biashara kipindi cha Julai- Septemba, 2024 na kubaini asilimia 64.35 ya wafanyabiashara hawakuwa na leseni za biashara.
Huku zaidi ya asilimia 90 ya wafanyabiashara walikuwa hawajalipa ushuru wa huduma (Service Levy) pamoja na ushuru wa nyumba za kulala wageni (Hotel Levy).
Takwimu hiyo imebainishwa Novemba 9,2024,na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Tanga Ramadhani Ndwatah,wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga,amesema hatua zilizochukuliwa ni kufanya uelimishaji kwa wadau juu ya matakwa ya sheria kuhusu ulipaji wa tozo hizo.
Amesema,katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024, Halmashauri ya Jiji la Tanga,limekusanya kiasi cha zaidi ya bilioni 1,9, sawa na asilimia 32.6 kupitia ushuru wa huduma (Service Levy), nyumba ya kulala wageni (Hotel levy) pamoja na ada za leseni za biashara (Business License Fee).Ikilinganishwa na kiasi cha zaidi ya 1.2,sawa na asilimia 22.6,kilichokusanywa kipindi Aprili hadi Juni 2024 katika vyanzo hivyo.
Pia amesema,taasisi hiyo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga,walifanya kazi ya kufika kwenye maeneo ya maduka,zahanati, hospitali,hoteli,vituo vya mafuta,bar,kumbi za starehe,shule,viwandani na sokoni katika kata zote za Halmashauri ya Jiji hilo.
Sanjari na hayo, amesema taasisi hiyo imeendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 41 yenye thamani ya bilioni 19.0,katika sekta kipaumbele ambazo ni elimu, barabara,mji na afya.Huku kupitia ofisi za Wilaya wameweza kufuatilia kwa ukaribu hatua za awali za miradi ya BOOST ,ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa ksmati zinazosimamia miradi hiyo.
Miradi 13,yenye thamani ya zaidi ya bilioni 11.8, imebainika kuwa na mapungufu kadhaa, kati ya miradi hiyo ,miwili imefunguliwa na majalada ya uchunguzi ambayo ni mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya maji (HTM) Wilaya ya Korogwe wenye thamani ya zaidi ya milioni 407 na ujenzi wa jengo la utawala lenye thamani ya bilioni 2.8.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato